ZANZIBAR-Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ametoa wito kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokubali kutumika vibaya kwa kununuliwa au kupokea rushwa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mheshimiwa Hemed ametoa kauli hiyo alipokutana na viongozi wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Kamati za Siasa za Majimbo na Wadi, katika mkutano uliofanyika katika Tawi la CCM Mahonda, Wilaya ya Kaskazini "B", Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha chama katika ngazi za msingi kuelekea uchaguzi.
Amesisitiza kuwa viongozi wa chama wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuweka mbele maslahi ya chama na kuwa tayari kujitolea kwa hali na mali katika kukitumikia Chama Cha Mapinduzi.
Ameonya dhidi ya vitendo vinavyokiuka maadili ya chama, vinavyoweza kuharibu taswira yake na kudhoofisha mshikamano wa ndani.
"Kipindi hiki tunapoelekea Uchaguzi Mkuu, ni lazima viongozi na wanachama wa CCM wawe wavumilivu, wastahimilivu na waepuke kabisa vitendo vinavyoweza kukitia doa chama chetu. Tuwe mfano wa kuigwa na vyama vingine kwa nidhamu na uwajibikaji,” alisisitiza Mh. Hemed.
Aidha, amewataka wajumbe watakaohusika na uteuzi wa wagombea kuhakikisha wanazingatia uaminifu, uadilifu na kuepuka maslahi binafsi ili chama kipate wagombea wenye sifa, uwezo na weledi wa kuwatumikia wananchi na kuleta ushindi wa kishindo kwa CCM.
Katika kuhamasisha ushiriki wa makundi mbalimbali, Mheshimiwa Hemed aliwahimiza wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza haki yao ya kikatiba na kushiriki katika ujenzi wa chama chao na taifa kwa ujumla.Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Ndugu Khamis Mbeto Khamis, alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imefanya maendeleo makubwa kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwaunga mkono Rais Dkt. Hussein Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili waendelee kuijenga Tanzania kwa mafanikio zaidi.


