ZANZIBAR-Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar imetoa wito kwa jamii kuhakikisha inatoa taarifa mapema wanapoona dalili au vitendo vyovyote vinavyoashiria ukatili dhidi ya wazee katika maeneo yao, kwa kuwasiliana na Sheha wa shehia husika.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Jumuiya hiyo, Bi. Salama Kombo Ahmad, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani inayotarajiwa kufanyika tarehe 25 Juni 2025.Bi. Salama amesema vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wazee vinaendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo, vikiwemo kunyanyapaliwa kwa tuhuma za ushirikina, kunyimwa huduma za afya katika vituo vya tiba, pamoja na kutengwa katika sehemu mbalimbali za utoaji huduma za kijamii.
“Wazee ni kundi lenye thamani kubwa katika jamii. Ni jukumu letu sote kuhakikisha wanaheshimiwa, wanatunzwa na wanalindwa dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa Jumuiya hiyo inaendelea kutoa mafunzo kwa wazee kuhusu namna ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, ambayo ndio yanawakabili zaidi, sambamba na kuwahimiza kufanya mazoezi ya mwili ili kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: "Wazee ni Hazina kwa Taifa-Tuwalinde, Tuwatunze."
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 25 Juni kwa lengo la kuwaenzi wazee, kutambua mchango wao kwa jamii, na kupinga aina zote za udhalilishaji, unyanyasaji na ubaguzi wanaokumbana nao.