Ajali yaua 28 Mbeya

MBEYA-Ajali iliyohusisha magari matatu ikiwemo lori na Coaster katika Mlima Iwambi jijini Mbeya imesababisha vifo vya watu 28 huku ikijeruhi wengine nane.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema ajali hiyo imetokea Jumamosi, Juni 7,2025 ambapo watu 27 walifariki papo hapo na majeruhi kuwahishwa Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo Mbalizi.‎‎

Amesema katika barabara kuu ya Tanzam kutokea Mbeya kwenda Tunduma, gari aina ya lori likiwa na tela likiendeshwa na dereva Philip Mwashibanda (33) liligonga magari mengine mawili.‎‎

Kamanda huyo amesema, katika magari hayo yaliyokuwa na abiria yaligongwa na lori hilo, kisha kutumbukia kwenye korongo lililopo Mto Mbalizi na kusababisha vifo na majeruhi hao.‎‎

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt.Juma Homera ametoa salamu za pole na kuwaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kuanzia leo kutengeneza barabara ya mchepuo iliyopo eneo la
Iwambi.

‎‎Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa wafiwa wote. Kupitia taarifa aliyoitoa kupitia mitandao yake ya kijamii, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameeleza kuwa,

"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya ndugu zetu 28 na majeruhi 8, vilivyotokana na ajali ya barabarani iliyotokea jana usiku katika Mlima Iwambi, kwenye Barabara Kuu ya Tanzania - Zambia, Mkoa wa Mbeya.

"Ninawaombea marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone haraka. Aidha, ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Juma Homera, familia zote za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyenzi Mungu awajalie subra na uvumilivu.

"Ninawasisitiza madereva kuendelea kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

"Nimeliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kikamilifu sheria za usalama barabarani, na pia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuendelea kuboresha hali ya barabara zetu, hasa maeneo yenye changamoto kubwa zaidi, kwa usalama wa watumiaji wote wa barabara,"ameeleza Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news