Hoja 15 za Muungano zapatiwa ufumbuzi chini ya Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali imepiga hatua kubwa katika kuzipatia ufumbuzi hoja 15 za Muungano.
"Katika kipindi hiki, tumepiga hatua kubwa, hususani kwa kuzipatia ufumbuzi jumla ya hoja 15 za Muungano, hatua inayozidi kuongeza imani ya Watanzania kwa Serikali."

Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Juni 27,2025 wakati wa hotuba ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

"Pamoja na hayo, niwaase Watanzania wenzangu, tuendelee kushikamana na kuwa makini na vitisho vyovyote dhidi ya Muungano wetu, na niwasihi kuendeleza umoja, utulivu na amani; vitu ambavyo ni sifa njema kwa nchi yetu."

Amesema,mafanikio hayo ni sehemu ya ahadi ambazo alizitoa baada ya kukabidhiwa dhamana ya kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kudumisha Tunu za Taifa ambazo ni amani, umoja na mshikamano, uhuru wa nchi yetu, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na kudumisha Muungano wetu.

"Kama ilivyokuwa kwa Serikali za Awamu zilizopita tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kujivunia tunu hizo na kuziimarisha.

"Nyote ni mashahidi wa namna nchi yetu ya Tanzania imeendelea kuwa nchi moja na Watanzania wanaendelea kuwa wamoja, wenye mashirikiano licha ya kuwa na tofauti zao za kidini, mila na desturi,itikadi za kisiasa na hata ushabiki wa michezo (Simba na Yanga).

"Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu kwa Bunge nilisisitiza umuhimu wa viongozi wa pande zote mbili za Muungano kukutana na kuzungumzia ustawi wa Muungano wetu.

"Nafurahi kuwataarifu kwamba maagizo yangu yale yametekelezwa kwa ufanisi zaidi chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais akisaidiwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news