DAR-Wadau wa sekta ya fedha nchini wametakiwa kuimarisha mbinu zao za usimamizi wa vihatarishi vya mikopo na kuhakikisha uadilifu katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku ili kulinda uthabiti wa mfumo wa fedha na kusaidia utoaji wa mikopo kwa njia salama na endelevu katika taasisi zao. 

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bw. Sadati Musa wakati wa ufunguzi rasmi wa warsha kuhusu usimamizi wa vihatarishi vya mikopo kwa maofisa wa mikopo kutoka mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha.
Bw. Sadati amepongeza juhudi za sekta hiyo katika kuboresha usimamizi wa hatari za mikopo, na kueleza kuwa kiwango cha mikopo chechefu (NPLs) kimeshuka kutoka asilimia 9.42 mwaka 2020 hadi asilimia 3.43 kufikia Mei 2025.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa bado kuna kazi ya ziada inayopaswa kufanywa na kila benki katika kuboresha mifumo yao ya udhibiti wa ndani na usimamizi wa vihatarishi.
Bw. Sadati ameelezea umuhimu wa kuwajengea wafanyakazi wa benki uwezo na kuwapa nyenzo sahihi za kupunguza hatari hizo kwa ufanisi huku akiwataka washiriki kutumia fursa hiyo kushiriki kikamilifu katika mijadala na kubadilishana uzoefu kwa vitendo ili kuimarisha uwezo wa pamoja wa sekta.
Warsha hiyo inayofanyika katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 16 hadi 20 Juni 2025, inatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa vihatarishi vya mikopo.



