Bodi ya Wakurugenzi ya BoT yafanya ziara ujenzi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato

DODOMA-Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, imefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.
Ziara hiyo iimefanyika leo Juni 17,2025 ambapo Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Kedrick Chawe, alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa chini ya usimamizi wa TANROADS kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Ujenzi huo unajumuisha njia ya kuruka na kutua ndege (runway), jengo la abiria, jengo la kuongozea ndege, pamoja na miundombinu mingine muhimu.
Kukamilika kwa uwanja huu kunatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kurahisisha usafirishaji wa mizigo, na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.

Aidha, mradi huu utaimarisha hadhi ya Dodoma kama mji mkuu na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.

Katika hatua nyingine, Bodi hiyo ilitembelea Kiwanda cha kutengeneza mvinyo wa zabibu cha CETAWICO kilichopo Hombolo, jijini Dodoma, ambako walipokelewa na Mkurugenzi wa Masuala ya Shirika, Bi. Katherine Mwimbe.
Alieleza kuwa, uwepo wa kiwanda hicho umeleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo kuongeza kipato cha wakulima wadogo kwa kununua zabibu zao na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 5,000 katika sekta ya kilimo kupitia zao la zabibu.

Kiwanda cha CETAWICO kinachangia kutangaza bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa kupitia mauzo ya mvinyo bora, hivyo kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo na kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.
Ziara hizo za Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania katika miradi ya kimkakati na shughuli za kiuchumi zinawawezesha kupata uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, changamoto zilizopo na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa ili kuwezesha maamuzi sahihi na yenye tija katika usimamizi wa sera ya fedha na maendeleo ya uchumi wa nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news