DCEA yafikisha elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa wananchi Kagera

KAGERA-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea na juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa wananchi wa Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Elimu hiyo imetolewa katika maeneo mawili muhimu ikiwemo Soko la Bunazi na eneo la Mutukula lililoko mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Tukio hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, ambapo Katibu Tawala wa Wilaya,Bi. Mwanaid Mang’uro alimwakilisha Mkuu wa Wilaya na kuongoza shughuli hizo muhimu.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya walihudhuria, jambo linaloonesha mshikamano wa pamoja katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Katika hamasa hiyo, wananchi walipewa elimu kuhusu athari za kiafya, kijamii na kiuchumi zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya.

Pia walihimizwa kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa pale wanapobaini vitendo vinavyohusiana na biashara au usambazaji wa dawa hizo haramu.
Kwa kutambua kwamba maeneo ya mipakani kama Mutukula ni hatarishi zaidi kwa usafirishaji wa biashara haramu ya dawa za kulevya, DCEA inaendelea kuweka mkazo katika kutoa elimu, kuongeza uelewa na kujenga ushirikiano na jamii kwa lengo la kuzuia uhalifu huo kuanzia ngazi ya chini kabisa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news