Deni la Serikali ni himilivu hatua zote-Waziri Dkt.Nchemba

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Dkt.Mwigulu Nchemba amesema,hadi Aprili 2025, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 107.70 kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 72.94 na deni la ndani ni shilingi trilioni 34.76.
"Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Oktoba 2024 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2024/25."

Ameyasema hayo leo Juni 12,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026.

Waziri Dkt.Nchemba amesema,thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55, thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 23.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40.

Vilevile amesema,thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.

Amesema,Machi 2025,Kampuni ya Moody’s Investors Service ilifanya zoezi la mapitio ya kwanza ya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa mwaka 2025.

"Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, kampuni hiyo ilichapisha matokeo ambayo yameendelea kuiweka Tanzania katika daraja la B1 kama ilivyokuwa kwa matokeo ya mwisho ya mwaka 2024.

"Aidha,kampuni nyingine kubwa ya Fitch Ratings inaendelea na mapitio ya kwanza kwa mwaka 2025 na inatarajia kuchapisha matokeo hivi karibuni."

Waziri Dkt.Nchemba amesema,kampuni hiyo ilichapisha matokeo ya mapitio ya mwisho Desemba 2024, ambapo iliiweka Tanzania katika daraja la B+.

Pia,amesema matokeo ya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa yanaendelea kuipa taswira chanya nchi yetu katika medani za kimataifa.

"Matokeo hayo ni bora kuliko nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Pamoja na mambo mengine,matokeo hayo yamechangiwa na jitihada za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi, kukuza uchumi,kusimamia kwa makini deni la Serikali na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa."

Wakati huo huo, Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha deni linaendelea kuwa himilivu ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo katika ugharamiaji wa bajeti.

Jambo lingine amesema ni kuelekeza fedha za mikopo katika miradi inayokuza mapato ya ndani na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.

Sambamba na kuendelea kuwahimiza maafisa
masuuli kuzingatia maandalizi ya msingi ya miradi kabla ya kuingia mikataba kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuepuka ongezeko la gharama za mradi unaokopewa fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news