Serikali ya Awamu ya Sita yavunja rekodi ukusanyaji wa mapato ya ndani

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha,Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa ambayo yameongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani.
"Ifahamike kuwa,kuimarika kwa makusanyo ya mapato ya ndani ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo,utoaji wa huduma bora kwa wananchi na ustawi wa Taifa kwa ujumla;

Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Juni 12,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026.

Amesema,katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mapato ya ndani yaliongezeka kutoka shilingi trilioni 20.59 mwaka 2020/21, sawa na wastani wa shilingi trilioni 1.72 kwa mwezi hadi shilingi trilioni 29.83 mwaka 2023/24, sawa na wastani wa shilingi trilioni 2.49 kwa mwezi.

Pia, Dkt.Nchemba amesema,katika kipindi cha Julai 2024 hadi Mei 2025,mapato ya ndani yamezidi kuongezeka kufikia wastani wa shilingi trilioni 2.83 kwa mwezi.

Vilevile,uwiano wa mapato ya ndani kwa Pato la Taifa umeongezeka kufikia asilimia 15.0 mwaka 2023/24 kutoka asilimia 13.7 mwaka 2020/21.

"Mwenendo huu chanya unadhihirisha mageuzi makubwa kwenye ukusanyaji wa mapato."

Waziri Dkt.Nchemba amefafanua kuwa, mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa sera madhubuti za bajeti na uimarishaji wa mifumo ya kiutendaji.

Jambo lingine ni matumizi sahihi ya mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) iliyounganishwa.

"Na kuimarisha uhusiano kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na walipakodi kupitia elimu ya mlipakodi, kampeni za uhamasishaji, na kuboresha huduma kwa wateja.

"Uboreshaji wa masoko ya madini, ambayo yameongeza mapato kutoka sekta ya madini kupitia tozo na ada mbalimbali na ufuatiliaji wa karibu wa mashirika ya umma,kuhakikisha kwamba yanaongeza tija,yanachangia gawio kwa Serikali, na hayatumii vibaya rasilimali."

Waziri Dkt.Nchemba amesema,kwa ujumla, mafanikio haya ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ni matokeo ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais hususani katika usimamizi madhubuti wa uchumi pamoja na jitihada za watumishi wa umma, taasisi za fedha, sekta binafsi, na wananchi kwa ujumla.

"Kipekee,napenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa taasisi zinazohusika katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Nianze kwa kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa usimamizi mzuri katika ukusanyaji wa mapato. Hakika TRA imefanya maboresho makubwa katika utendaji wake ambayo yamesaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.Kodi yetu, Maendeleo yetu."

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba ameipongeza Wizara ya Madini kwa kusimamia ipasavyo sekta ya madini ambayo imekuwa chanzo muhimu cha mapato pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa usimamizi madhubuti wa mapato yanayokusanywa na mamlaka za Serikali za mitaa.

Amesema,jitihada zao zimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio tunayoyaona leo katika eneo la mapato ya ndani.

Waziri Dkt.Nchemba pia ametoa rai kwa taasisi
nyingine za Serikali zenye dhamana ya kukusanya mapato ziige mfano wa wizara na taasisi hizi kwa kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ili tuondokane na utegemezi wa bajeti.

Pia,amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuboresha sera,mifumo na mbinu za ukusanyaji mapato ili kufikia azma ya kujitegemea.

"Niwahakikishie kuwa, Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayekwamisha azma hii."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news