Hazina yawalipa wastaafu na warithi shilingi bilioni 315.08 za mafao

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwingulu Nchemba amesema,hadi kufikia Aprili,2025 wizara imelipa kwa wakati shilingi bilioni 315.08 kama mafao ya kiinua mgongo kwa wastaafu na warithi wanaolipwa na Hazina.
Amesema, wizara ilifanya hivyo baada ya kupokea nyaraka kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ikiwa pia ni utekelezaji wa mipango yake kwa mwaka 2024/25.

Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Juni 4,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025|2026.

"Aidha, michango ya kisheria ya kila mwezi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii iliwasilishwa kwa wakati na malipo ya kila mwezi ya pensheni ya mifuko ya hifadhi ya jamii yalifanyika kwa wakati baada ya kupokea hati za madai."

Elimu ya Fedha

Pia,Waziri Dkt.Nchemba amesma,katika mwaka 2024/25, wizara ilipanga kuendelea kutekeleza programu ya elimu ya fedha kwa kutoa elimu ya fedha kwa lengo la kujenga uelewa na kuongeza maarifa ya masuala ya fedha kwa umma na kukuza huduma jumuishi za fedha nchini.

Amesema,hadi Aprili 2025, elimu ya fedha ilitolewa katika halmashauri 61 za mikoa ya Lindi, Mtwara, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Mwanza, Mara na Pwani ambapo jumla ya wananchi 49,271 walipatiwa elimu kuhusu huduma jumuishi za fedha.

"Jumla ya wananchi 3,419 walipatiwa elimu ya huduma za fedha kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Mkoa wa Mbeya."

Vilevile, amesema wizara imeendelea kutekeleza Mkakati wa Upatikanaji wa Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa mwaka 2023/24-2028/29 kwa lengo la kuongeza wigo wa vyanzo vya mitaji kwa wajasiriamali, ambapo wajasiriamali 640 kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani, Mtwara, Lindi na Tanga wamepatiwa mafunzo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news