BoT itaendelea kusimamia utulivu wa uchumi,kulinda thamani ya Shilingi-Waziri Nchemba

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha imesema, kwa mwaka 2025/26, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepanga kudhibiti mfumuko wa bei usizidi asilimia tano na kuhakikisha utulivu wa uchumi ikiwemo kudhibiti viwango vya riba ili kuakisi mahitaji ya ukwasi katika soko.
Waziri wa Fedha, Mhe.Dkt.Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo Juni 4,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2024/25 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka 2025/26.

Vilevile, amesema BoT itaendelea kudhibiti akiba ya fedha za kigeni ili kuwezesha uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Sambamba na kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya sarafu za kigeni ikiwemo kuboresha mifumo ya malipo ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu nchini.

Waziri Dkt.Nchemba amesema, pia kwa mwaka 2025, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imepanga kuzalisha mapato ya shilingi bilioni 69.53 na kukuza faida ya benki kabla ya kodi shilingi bilioni 30.65 kutoka shilingi bilioni 24.68 kwa mwaka 2024.

Amesema, benki hiyo itaendelea kutoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 300 ikilinganishwa na shilingi bilioni 286.38 kwa mwaka 2024.

"Na kuongeza thamani ya mali za benki kufikia shilingi trilioni 1.13 kutoka shilingi bilioni 917.41 kwa mwaka 2024 ikiwemo kufuatilia marejesho ya mikopo shilingi bilioni 120."

Pia,kwa mwaka 2025,Waziri Dkt.Nchemba amesema,Benki ya Maendeleo (TIB) imepanga kutoa mikopo ya shilingi bilioni 20 na kuongeza mali za benki hadi shilingi bilioni 478 kutoka shilingi bilioni 453 mwaka 2024.

Amesema, mwaka ujao benki hiyo itakusanya marejesho ya mikopo iliyo nje ya mizania ya benki shilingi bilioni 11.14 na mikopo iliyo ndani ya mizania ya benki shilingi bilioni 25.03.

"Kwa mwaka 2025, Benki ya Biashara Tanzania imepanga kuzalisha mapato ya shilingi bilioni 316, kukuza faida ya benki kabla ya kodi ya shilingi bilioni 65 na kutoa mikopo ya shilingi bilioni 1,483."

Vilevile ameeleza kuwa,benki hiyo inatarajia kukusanya amana za wateja shilingi bilioni 1,858 na kukuza mali za benki hadi shilingi bilioni 2,274 kutoka shilingi bilioni 1,738 mwaka 2024.

Jambo lingine amesema ni kukuza mtaji wa benki hadi shilingi bilioni 193 kutoka shilingi bilioni 151 mwaka 2024 na kuongeza idadi ya wateja hadi 1,214,059 kutoka wateja 914,059 mwaka 2024.

Waziri Dkt.Nchemba akizungumzia kuhusu Mfuko wa Huduma Ndogo za Fedha (SELF) kwa mwaka ujao amesema,umepanga kutoa mikopo ya shilingi bilioni 48 kutoka shilingi bilioni 45.2 mwaka 2024.

Mfuko huo, pia unatarajiwa kukuza faida kabla ya kodi hadi shilingi bilioni 1.14 kutoka shilingi bilioni 1.09 mwaka 2024 na kukuza mtaji hadi shilingi bilioni 61.0 kutoka shilingi bilioni 58.99 mwaka 2024.

Amesema,matarajio mengine ni kuongeza idadi ya wateja hadi 60,000 kutoka wateja 55,743 mwaka 2024 na kukusanya marejesho ya mikopo iliyo nje ya mizania ya mfuko shilingi bilioni 2.0 kutoka shilingi bilioni 1.49 na mikopo iliyo ndani ya mizania shilingi bilioni 53.05 kutoka shilingi bilioni 41.63 mwaka 2024.

Waziri Dkt.Nchemba amesema, mfuko pia unatarajiwa kuzalisha mapato ya jumla ya shilingi bilioni 12.13 kutoka shilingi bilioni 8.32 mwaka 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news