Lazima mali za umma tulizokabidhiwa ziwe na matokeo chanya-Msajili wa Hazina

NA GODFREY NNKO

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema, mageuzi na mabadiliko ya kifikra katika kuendesha taasisi na mashirika ya umma ni nguzo muhimu ili kuleta ufanisi, uwajibikaji na maendeleo endelevu nchini.
"Kwa hiyo, katika taasisi zote lazima kuwe na mabadiliko chanya kuhakikisha mali tulizokabidhiwa zinakuwa na matokeo chanya."

Mchechu ameyasema hayo leo Juni 2,2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kifungua kinywa (breakfast meeting) uliowakutanisha pamoja viongozi, wahariri na waandishi wa habari.

Mkutano huo umeangazia safari ya mageuzi, mafanikio, mikakati na uelekeo wa taasisi na mashirika ya umma yaliyopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Mchechu amesema, mageuzi ndani ya mashirika na taasisi huwezesha kubadili mifumo isiyofanya kazi na kuimarisha utendaji bora wa huduma kwa wananchi na kuongeza mapato.
Pia, amesema mabadiliko ya kifikra yanasaidia viongozi na watumishi wa mashirika kufikiria kwa njia mpya, kuwa wabunifu na kuondokana na mazoea duni ya kufanya kazi.

Vilevile, Msajili wa Hazina amesisitiza kuwa, ofisi yake imedhamiria kuhakikisha inaeneza mageuzi chanya yanayochochewa na mabadiliko ya kifikra ili kuongeza uwazi, ushirikishwaji na mawasiliano bora kutoka katika mashirika na taasisi za umma.

Msajili wa Hazina amesema kuwa,kupitia mageuzi yanayosimamiwa na ofisi yake yameleta matokeo chanya ikiwemo muundo mpya wa ofisi.

Amesema, muundo mpya uliidhinishwa Julai,2023 ambapo nafasi muhimu hadi kufikia Oktoba, 2023 zilijazwa.

Hatua hiyo, Msajili wa Hazina amesema, imewezesha ofisi ya TR kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
"Tunaendelea na maandalizi ya mpango mkakati wa muda mrefu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina."

Vilevile, Mchechu amesema mageuzi hayo yamewezesha taasisi 57 kujiendesha kwa uhuru ili kufikia ufanisi uliotarajiwa wakati wa uanzishwaji.

"Pia, tumeweza kuunganisha taasisi 14 na kuunda taasisi sita, na kufuta taasisi tatu."

Katika hatua nyingine, Mchechu amesema kuwa, kupitia mageuzi hayo wameweza kuboresha mizania za taasisi.

Amesema, wamefanikiwa kuongeza mtaji wa Benki ya TCB kiasi cha shilingi bilioni 131 na kutengeneza faida ya shilingi bilioni 31.6 mwaka 2024.

Vilevile,Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongezewa shilingi trilioni 2.4 na kuwezesha ongezeko la faida kutoka shilingi bilioni 0.9 hadi kufikia shilingi bilioni 21.8 mwaka 2024.

Mchechu ameongeza kuwa, kwa upande wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) waliweka shilingi trilioni 2.7 ambapo ongezeko la faida lilitoka shilingi bilioni 159.6 hadi shilingi bilioni 306 mwaka 2023/2024.

Gawio Day 2025

Msajili wa Hazina,Mchechu akizungumzia kuhusu Siku ya Gawio (Gawio Day) ambayo imeasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, imeleta ari na hamasa kwa taasisi na mashirika ya umma kwa kila moja kutaka kushiriki kikamilifu kutoa gawio.
Ameeleza kuwa, kabla ya Juni 10,2025 ambayo ni Siku ya Gawio tayari shilingi bilioni 900 zimekusanywa huku matarajio yakiwa ni zaidi ya shilingi trilioni moja ambazo zitakabidhiwa kwa Rais Dkt.Samia kama michango na gawio kwa Serikali.

"Kwa hiyo Juni 10,2025 taasisi na mashirika ya umma yatamkabidhi rasmi Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan michango na gawio kwa Serikali, Ikulu jijini Dar es Salaam."

Mchechu amesema kuwa, Siku ya Gawio si tu alama ya uwajibikaji bali ni kama chombo cha kutathmini utendaji kazi wa mashirika na taasisi za umma kwa mujibu wa malengo ya Taifa.

"Siku ya Gawio imekuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi na mafanikio tunayoyaona leo."

Msajili wa Hazina amesisitiza kuwa,tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo wa wazi na wenye uwajibikaji kumekuwa na ongezeko la mashirika yanayotoa gawio na kuboresha utendaji kazi wao.

"Hii ni ishara kuwa,pale ambapo taasisi za umma zinasimamiwa kwa weledi,mafanikio ya kweli yanawezekana."
Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) inasimamia mashirika na taasisi 308 huku kati ya hayo, mashirika ya umma ni 253 ambapo 35 yanafanya biashara na 218 yasiyo ya biashara.

Serikali, pia ina hisa chache kwenye mashirika 56 ambapo 46 yapo ndani ya nchi na 10 nje ya nchi yote yakiwa yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news