Mkalama yarejesha tabasamu kwa wazee

SINGIDA-Jumla ya wazee 20 kutoka Wilaya ya Mkalama wamekabidhiwa kadi za msamaha wa matibabu bure wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili kwa Wazee Duniani kwa Mkoa wa Singida, yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Sheketela uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali, aliwataka wazee kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kusimamia maadili na malezi bora ya watoto, pamoja na kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

“Tunayoyaona leo ni matokeo ya malezi yetu. Tulishindwa kuwasimamia watoto wetu vizuri, matokeo yake tunaona baadhi ya watoto wamewatelekeza wazee wao,” alisema Mhe. Machali.
“Nitumie nafasi hii kuwahimiza wazee kuwasimamia watoto wao wenye watoto katika malezi, ili tuepukane na changamoto kama hii.”

Mhe. Machali aliwakumbusha wazee kutumia ofisi za Ustawi wa Jamii zilizopo katika halmashauri zao kama njia rasmi ya kuripoti vitendo vya unyanyasaji na ukatili wanavyofanyiwa, badala ya kuvumilia kimya kimya hali zinazowakandamiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Singida, Mchungaji Mbura Joel, alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zinazofanyika katika kulinda haki na ustawi wa wazee nchini.
Akizungumza kuhusu kadi hizo za msamaha wa matibabu, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mkalama, Bi Mwajuma Yusuphu, alisema kuwa kadi 20 zilizotolewa leo ni sehemu ya jumla ya kadi 5,000 zilizotolewa kwa wazee mbalimbali wilayani humo kuanzia Julai 1, 2024 hadi Juni 2025.

Maadhimisho hayo yalilenga kuhamasisha jamii kutambua, kulinda na kutetea haki za wazee sambamba na kuhakikisha kuwa kundi hilo linaishi kwa heshima, usalama na upendo katika familia na jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news