Mlio kuliko vita,hebu rudini nyumbani

NA LWAGA MWAMBANDE

KUNA methali ya kiswahili inabainisha kuwa, mafahari wawili wagombanapo ziumiazo ni nyasi. Ni kwa msingi kwamba, wakubwa wawili wanapogombana, wanaoumia zaidi ni watu wa kawaida wasiokuwa na hatia ndani na nje.
Kilichotokea usiku wa Alhamisi ya Juni 12, 2025 kuamkia Ijumaa ya Juni 13, kwa Israel kuishambulia Iran, shabaha ikawa maeneo ya kijeshi na serikali, bado kinasababisha vichwa vya wengi kujaa tafakari nzito.

Hivyo,katika muktadha wa vita kati ya Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, methali hii inadhirisha wazi kuwa,mgogoro wa mataifa haya mawili yenye nguvu kijeshi,ushawishi wa kisiasa na kiuchumi duniani madhara yake yanaweza kuwa makubwa zaidi duniani.

Kila mmoja wetu ana kumbukumbu kuhusu namna ambavyo mapigano ya Urusi na Ukraine yalivyotikisa uchumi wa dunia. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, amani ni kila jambo duniani. Endelea;

1.Mlio kuliko vita, hebu rudini nyumbani,
Subiri iishe vita, ndio mwende ugenini,
Habari tunazopata, hali huko mashakani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

2.Makombora tunaona, yanavyoruka hewani,
Uharibifu twaona, watu wenda mautini,
Wenyewe wanapigana, kwetu yatanda amani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

3.Mliko Watanzania, Israeli na Irani,
Tunajua yenu nia, mwafanya yenye thamani,
Walakini angalia, siingie msambweni,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

4.Iwe mnasoma shule, mkiwako ugenini,
Au kazi vilevile, pesa ziwe mfukoni,
Sasa hali tete kule, rudini kwanza nyumbani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

5.Tunaishi mara moja, hapa kwetu duniani,
Hii kubwa sana hoja, kuitafuta amani,
Wasijewavunjavunja, sisi tuwe kilioni,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

6.Kusikia la mkuu, muhimu sana jamani,
Yasije kuja makuu, tubakie macho chini,
Watu wavunjike guu, wanaswe huko vitani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

7.Ameagiza Rais, walioko ugenini,
Ambao huko wahisi, wanaishi hatarini,
Waondoe wasiwasi, kwa kurejea nyumbani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

8.Asante Mama Samia, kiongozi wa nyumbani,
Raia kuangalia, waishio ugenini,
Wasije kuangamia, maeneo ya vitani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

9.Kunakopiganwa vita, kwa makombora hewani,
Busara iweze pita, wote wakae mezani,
Yanayoleta utata, yaishe kuwe amani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

10.Kurushiana silaha, ni athari duniani,
Mara sote tutahaha, uchumi uende chini,
Hii ya kwetu furaha, ififie iwe duni,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

11.Amani kamwe haiji, ncha ya panga hewani,
Bali inachohitaji, ni watu wakae chini,
Wajadili mahitaji, na kufikia mwishoni,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

12.Dunia ni yetu sote, tukalie kwa amani,
Kuhasimiana kote, hakufai maishani,
Tuheshimiane sote, na itawale amani,
Wito mkuu wa nchi, ni vema ukaenziwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news