DAR-Klabu ya Simba SC imesema ipo tayari kwa Derby ya Kariakoo kati yao na Yanga Sc itakayopigwa Juni 15,2025 huku ikiwataka mashabiki wakaujaze Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Klabu ya Simba inatoa taarifa kwa Wanachama, Wapenzi, na Umma kuwa mchezo nambari 184 dhidi ya Yanga uliopangwa kufanyika tarehe 15/6/2025 upo kama ulivyopangwa.
"Tunawasihi msihadaike na kelele za mitaani, Wale ambao walinunua tiketi za mechi ya tarehe 8/3/2025 wazitunze kwa ajili ya matumizi ya mchezo huo na wale ambao hawajanunua tiketi wajiandae kununua baada ya tangazo la Bodi ya Ligi.
Twendeni tukaujaze Uwanja wa Mkapa.
"Inafahamika wazi kuwa Ligi Kuu ya NBC inajumuisha Timu 16 na si ligi ya timu moja, kwa mujibu wa taratibu kabla ya kuanza msimu,vilabu vyote 16 hushiriki vikao na kutoa mapendekezo ya kuboresha kanuni na taratibu ili kuimarisha ligi yetu,hivyo wenye hoja wafuate taratibu husika.
Tunaomba Bodi ya Ligi na TFF watoe hadharani ripoti ya uchunguzi juu ya wale wote waliohusika kuharibu mechi ya ligi jioni ya tarehe 7/3/2025 na wachukuliwe hatua stahiki na mamlaka husika.
Kutotolewa kwa ripoti na kutochukuliwa hatua kwa wanaoendelea kuchochea ghasia ni sawa na kulinda uharamia katika mpira ambao unatia dosari mafanikio yaliyopo katika tasnia ya mpira wa miguu nchini kwa sasa.”