NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC), Bw. Hamad Abdallah amesema, katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan shirika hilo limejenga nyumba 5,399 zenye thamani ya shilingi bilioni 659.48.
Muonekano wa nyumba za mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) uliopo Kawe jijini Dar es Salaam leo Juni 16,2025.
Nyumba hizo ni kwa ajili ya kuuza na kupangisha ambapo nyumba 3,217 ujenzi wake umekamilika na nyumba 2,182 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2026.
Bw.Abdallah ameyasema hayo leo Juni 16,2025 katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri Tanzania ulioambatana na ziara maalum ya miradi inayotekelezwa na shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Pia, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema,shirika linaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nyumba za makazi ikiwemo ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati na chini kupitia mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) ambao utekelezaji wake unaendelea.
"Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba bora nchini.
"Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine."
Wahariri katika ziara ya mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) uliopo Kawe jijini Dar es Salaam wameonesha kuvutiwa na kazi nzuri ambayo inafanywa na NHC ambapo licha ya kupongeza,pia wameonesha shauku ya kununua nyumba awamu ijayo.
SHS ambao ni mradi mkubwa wa makazi ya kisasa umekamilika kwa asilimia 100, na tayari wateja wanatarajiwa kukabidhiwa nyumba zao mwezi ujao.
Aidha,jumla ya nyumba 560 zimejengwa kwa viwango vya juu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora na ya kisasa nchini.
Gharama za ujenzi ni shilingi bilioni 48.32 ambapo hadi sasa shirika limeshatumia kiasi cha shilingi bilioni 39.
Vilevile,mradi huo umesanifiwa, kujengwa na kusimamiwa na kurugenzi za ujenzi na usanifu za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Kawe 711
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, amesesema kuwa,Mradi wa Kawe 711 wenye thamani ya shilingi bilioni 169 umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Aprili, 2026.
"Natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kupata kibali cha kukopa shilingi bilioni 174 mwaka 2023.
"Fedha hizi zimesaidia kukamilisha Mradi wa Morocco Square uliokuwa umesimama kwa miaka mitano na kuanza ujenzi wa Kawe 711."
Vilevile, Bw.Abdallah amesema,Mradi wa Golden Premier Residence(GPR) wenye thamani ya shilingi Bilioni 127 uliopo Kawe, mazungumzo kati ya mkandarasi na shirika yamekamilika na ujenzi unaendelea na utakamilika Septemba,2027.
Kwa nyakati tofauti Wahariri walionesha kuguzwa zaidi na dhamira ya thabiti ya Serikali kupitia NHC hasa kuamua kuikwamua miradi hiyo ambayo ilikwama.
Mathalani, mradi wa GPR ambao ulikwama kwa miaka nane, Wahariri wameshuhudia timu ya wataalamu ikiwa kazini kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo
GPR umeanza upya kwa kasi baada ya kupatikana kwa mkopo kwa idhini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kariakoo
Wakati huo huo, Bw.Abdallah amesema, shirika hilo limeanza rasmi utekelezaji wa mpango mkubwa wa kuibadilisha sura ya eneo la Kariakoo kwa kuondoa majengo chakavu na kuijenga majengo ya kisasa yanayolingana na mahitaji ya sasa ya makazi, biashara na maendeleo ya miji.
Amesema kuwa, ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo,shirika hilo linatarajia kuvunja na kujenga upya majengo yote chakavu ya NHC yaliyopo Kariakoo na kuyaweka kwenye hadhi mpya ya majengo ya kisasa ya kuanzia ghorofa 10 hadi 15.
Kupitia mpango huo, amesema hawatakuwa tena na jengo chakavu la shirika hilo ndani ya Kariakoo.
Amesema,tayari wameanza na miradi 16 ambapo majengo ya zamani yamevunjwa na ujenzi wa majengo mapya unaendelea.
"Kwa ujumla, majengo 64 yataondolewa na kujengwa upya kama sehemu ya mageuzi haya ya kimkakati."
Amesema, miradi hiyo inatekelezwa kwa mfumo wa ubia baina ya NHC na sekta binafsi, pamoja na ujenzi unaofanywa moja kwa moja na shirika lenyewe.
“Ni muda wa kufanya matumizi bora ya ardhi, hasa katika maeneo ya kibiashara kama Kariakoo.
"Tunataka kila kipande cha ardhi ya NHC kitumike kwa tija zaidi, na kwa namna inayolipa kiuchumi na kijamii. Majengo haya mapya hayatakuwa tu ya makazi, bali yatachanganya biashara, huduma, ofisi na maeneo ya kijamii."
Kuhusu NHC
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liliundwa upya kupitia Sheria ya Bunge Na. 2 ya mwaka 1990 kwa kuunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba lililoanzishwa mwaka 1971 kwa sheria Na. 13.
Kupitia Sheria ya mwaka 1990, Bw.Abdallah amesema, Shirika la Nyumba la Taifa lilikabidhiwa mali zote za Msajili wa Majumba.
"Baadaye sheria hii, ilirekebishwa kupitia Sheria ya Marekebisho (Miscellaneous Amendments Law) Na. 2 ya mwaka 2005 ambayo imerekebishwa tena mwaka 2025."
"Marekebisho hayo yaliyohusu marekebisho ya Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na kufuta Sheria ya Udhibiti wa Kodi za Pango la Nyumba (Rent Restriction Act) Na. 17 ya mwaka 1984.
"Marekebisho ya sasa (2025) yamelenga kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake kiufanisi zaidi kwenye mazingira ya ushindani wa kibiashara katika soko la miliki."
Tags
Ardhi
Breaking News
Habari
Mikoa ya NHC
NHC Morocco Square
NHC Tanzania
Sera ya Ubia NHC
Shiri la Nyumba la Taifa (NHC)




