DAR-Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea na juhudi za kupambana na vitendo vya kihalifu sambamba na kushirikiana na umma katika kuhakikisha usalama unaimarika jijini humo.
Katika kipindi cha Januari 2023 hadi Mei 2025, jeshi hilo limewakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa mbalimbali wa makosa ya jinai, ambapo baadhi yao tayari wamehukumiwa vifungo mbalimbali.
KESI ZA UBAYA WA KINGONO
Katika makosa ya kubaka, jumla ya washukiwa 10 wamefungwa, wakiwemo:
Salum Mohamed, aliyepatikana na hatia ya kubaka Mbagala mwaka 2023 na kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Fadhili Fredrik, Ezra Dikson, Said Haji Muhita, Selemani Shafii, Nassoro Mkulwa wote wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Said Hashim Athuman, Aden Sanilo Balinzo, Steven Charles, na Athumani Hamis Chambila wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 kila mmoja.
Kwa upande wa kesi za kulawiti, watuhumiwa 8 wamehukumiwa, akiwemo: Baraka Modestus, Baraka Benedicto, Selemani Shafii, Dotto Athumani, Maneno Mwandumbya, na Omar Kheri waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Msafiri Baraka Abdallah alihukumiwa kifungo cha miaka 30. Selemani Shafii pia alipatikana na hatia ya kosa lingine la kulawiti na kuhukumiwa kifungo cha maisha.
KESI ZA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA
Watuhumiwa tisa wa unyang’anyi wa kutumia silaha walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa, wakiwemo:
Ally Bakari Tengatenga aliyepatikana na hatia ya unyang’anyi Mbweni Kijijini na kuhukumiwa kifungo cha miaka 60. Omar Yahaya Lwavu alihukumiwa kifungo cha maisha.
Watuhumiwa wengine, akiwemo Felix John Msangi, Boniface Elias (Tuface), Adam Sanila Balinzigo, Ali Said Omar na Said Abdala pamoja na wenzao, walihukumiwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja.
USALAMA BARABARANI
Katika kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinatekelezwa ipasavyo, Jeshi la Polisi limefanya operesheni maalum kuanzia Aprili hadi Mei 2025, ambapo jumla ya watumiaji wa barabara waliokamatwa kwa makosa ya kuendesha vyombo vya moto katika barabara za mwendokasi ni:
■Madereva wa magari ya Serikali: 35
■Magari binafsi: 123
■Pikipiki (bodaboda): 61
■Bajaj: 65
■Wengine 41 walionywa
Aidha, jumla ya madereva 19 walikamatwa kwa kuendesha wakiwa wamelewa, ambapo madereva 14 wamefikishwa mahakamani, 3 wamefungiwa leseni, na 2 waliandikiwa faini.
Kati ya waliokamatwa, madereva 16 walikuwa wa magari binafsi na 3 walikuwa wa magari ya abiria ambao wanakabiliwa na makosa chini ya sheria ya Usalama Barabarani (Sura ya 168) na Kanuni za Usafiri wa Umma (GN No.81 ya mwaka 2020).
WITO KWA UMMA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu, pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kulinda maisha na mali.
Jeshi linaahidi kuendelea na juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama kwa ustawi wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
