Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa Jeshi la Polisi

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linaimarisha maadili kwa vitendo kwa maafisa na askari wake ili kulinda heshima ya taasisi hiyo na kuzidi kujenga imani ya wananchi kwa vyombo vya dola.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo Juni 9,2025 katika sherehe za kufunga Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi Na. 1 ya Mwaka 2024/2025 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA) Kurasini, ambapo jumla ya wahitimu 955 walitunukiwa vyeti baada ya kuhitimu mafunzo yao ya miezi tisa.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema mafanikio ya Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao
hayawezi kupatikana endapo maadili yataendelea kudorora miongoni mwa watendaji
wake, huku akisisitiza kuwa nidhamu, uadilifu na uaminifu kwa umma ni msingi imara wa kuijenga taasisi ya Polisi inayoaminika na kuheshimiwa na wananchi.
Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amewataka wahitimu hao kuzingatia viapo vyao vya kazi,kuepuka vitendo vya rushwa na kuwa kielelezo cha mabadiliko chanya na maboresho ya kiutendaji kwenye maeneo yao ya kazi.

Akizungumzia usalama barabarani, Rais Dkt. Samia ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha mikakati ya kudhibiti ajali za barabarani, akisema licha ya kushuka kwa jumla ya idadi ya ajali na vifo katika mwaka mmoja uliopita, bado takwimu za vifo ni kubwa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kudhibiti ajali hizo kwa ufanisi zaidi.

Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA, vifaa vya kisasa na rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya usimamizi wa usalama barabarani, mashauri ya jinai, na taarifa za mali zilizopotea ili kurahisisha utendaji kazi.
Vile vile, amesisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi, wananchi,vyombo vingine vya dola na taasisi za usalama za nje ya nchi, kwa kuwa vitisho vya kiusalama vinazidi kuvuka mipaka sambamba na kukua kwa uhalifu wa kidijitali.

Ameagiza pia mafunzo kazini yazingatie hali halisi ya sasa ili kuimarisha utayari wa askari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news