Salamu za Jumapili:Kama unatenda haki…

NA LWAGA MWAMBANDE

MWANAZUONI wa Kigiriki,Aristotle katika maandiko yake amewahi kunukuliwa akisema kuwa,haki ni kutoa kwa kila mtu kile anachostahili.
Aristotle alitofautisha kati ya haki ya usawa mgawanyo wa mali au nafasi kwa misingi ya mchango au stahili ya mtu.

Vile vile aliangazia haki ya kurekebisha makosa au madhara yaliyotokea kati ya watu.

Kwa msingi huo haki ni uwezo au uhuru mtu ambao anao kisheria au kimaadili wa kufanya au kupata kitu fulani.

Hivyo haki zina umuhimu katika maisha yetu ya kila siku kwa sababu zinalinda utu wa binadamu na kuwezesha usawa katika jamii.

Pia,haki zinazuia dhuluma na unyanyasaji ikiwemo kuwezesha amani,umoja,mshikamano katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Ukirejea katika maandiko matakatifu utaona kuwa,haki imewekewa mkazo mkubwa mfano katika kitabu Kitakatifu cha Mathayo 12:37,13:49 ukisoma utaona neno la Mungu linasema,

...Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.

...Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki...

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kama ukitenda haki,kumbuka mwisho wako ni mzuri.Endelea;

1. Watu wengi vifo vyao, huakisi siku zao,
Yaani maisha yao, na mingi miaka yao,
Ama ni neema kwao, pengine laana kwao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

2. Mfano watenda haki, jinsi wawaonya wao,
Ukasababisha chuki, ikazuka kati yao,
Hakikisha hubandiki, uwape furaha wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

3. Hata kichwa wakukate, hiyo ni shauri yao,
Pumzi ya mwisho uvute, wapate furaha wao,
Tukuone tusijute, kwa huo unyama wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

4. Au wakupige mawe, hizo mahakama zao,
Kwa sana uchafuliwe, kwa kuwa kinyume chao,
Walakini uelewe, kweli huna chuki nao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

5. Watashangilia wao, kwa hayo matendo yao,
Kwamba kifo chako kwao, yawa ni amani yao,
Wanajidanganya hao, Mungu wako siyo wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

6. Na wala hawajashinda, wanavyofikiri wao,
Kwamba yako yamepinda, vile wamebaki wao,
Wewe kule umekwenda, kuzuri kuliko wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

7. Haki itakuinua, licha ya madhira yao,
Dunia itatambua, wataofutika wao,
Mungu atakuchukua, wataobaki ni wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

8. Kila siku sema kweli, ni ujumbe wako kwao,
Lengo ni kuwabadili, waziache njia zao,
Zilojaa ubatili, kwa maangamizi yao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

9. Mungu akusaidie, usiwafwatishe wao,
Mungu ndiye msikie, aseme kuhusu wao,
Kweli kwako ibakie, hata wasitake wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

10. Yohana Mbatizaji, kwa Mungu yake makao,
Japokuwa wauaji, walimfanyia yao,
Kweli ni wake mtaji, alowaambia wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

11. Stefano twamjua, kufia dini ni zao,
Yesu aliyemjua, aliwaambia wao,
Wakaona azingua, akafa kwa mawe yao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

12. Tamani ishi vizuri, usiwafuate wao,
Injili ya Mungu kiri, tena uwaonye wao,
Wakisikia vizuri, dharau hasara kwao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.

13. Utamani mwisho mwema, kwake Mungu siyo kwao,
Fuata anayosema, wala si matakwa yao,
Hata kuwe na mlima, huo si wako ni wao,
Kama unatenda haki, mwisho wako ni mzuri.
(Marko 6:17-28, Matendo ya Mitume 6:8-15, 7:52-60)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news