DAR-Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limesema mfumo wa vyama vingi haupo kwa ajili ya kujengeana uadui au kuanza kukashfiana bila kutoa hoja za msingi zinazoweza kuchochea misingi ya maendeleo ya nchi.
Akiwasilisha salamu Juni 7,2025 kwenye Baraza la Eid El-Adh'haa katika msikiti wa Mfalme Mohamed VI BAKWATA makao makuu Dar es Salaam, Katibu Mkuu Alhaj Nuhu Mruma,amesema Tanzania ni nchi yenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
"Mfumo huu ni mfumo wa ushindani wa hoja za kimaendeleo na hatimaye kushika au kuogoza dola au uongozi wa nchi,"amesema.
"Tunaendelea kuviasa Vyama vyote vya siasa kuendesha siasa za kistaarabu na kujenga kuvumiliana katika tofauti zetu za kisiasa na itikadi na kamwe zisipelekee kuwagawanya wananchi,"amesema.
Sheikh Mruma amesema wao kama viongozi wa dini wataendelea na jukumu la kuiombea nchi amani na kuwaombea viongozi wote pamoja na kuendela kuwashauri katika mambo mbalimbali yenye tija katika nchi.
"Tunawaomba viongozi wetu wakuu wa nchi waendelee kuuamini mhimili huu muhimu wa taasisi za dini na kuutumia ili kuleta mustakabali mwema baina ya viongozi na wananchi,"amesema.
Aidha, amewasihi viongozi wa dini kutumia vizuri majukwaa ya nyumba za ibada kueneza mafunzo mazuri ya dini zetu yanayotokana na maandiko muhimu ya vitabu vitakatifu na kuepuka kuhubiri siasa kwa kuwa kunaweza kuwachanganya waumini ambao wana itikadi zao tofauti.
