Sekta ya Utalii ina mchango mkubwa kwa Taifa-Dkt.Biteko

ARUSHA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Dotto Biteko amesema kuwa,sekta ya utalii imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa maliasili na malikale, ustawi wa jamii na ukuaji wa kiuchumi nchini.
Ameyasema hayo leo Juni 6,2025 katika viwanja vya Magereza jijini Arusha wakati akifungua Onesho la Utalii la Kimataifa la Karibu Kilifair 2025.

"Mfano, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa, sekta hii inachangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya mauzo ya nje."

Aidha,Dkt.Biteko amesema,utalii ni biashara inayofunganisha huduma, vivutio mbalimbali vikiwemo, mandhari ya kuvutia na ukarimu wa Watanzania, ikisimulia hadithi ya kipekee ya urithi wa kitamaduni na uvumbuzi wa kisasa ambapo makundi mbalimbali ya wageni hupata fursa ya kuvinjari na kufurahi.
Amesema,kwa kutambua umuhimu wa utalii, Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza programu mbalimbali za kimkakati za utangazaji utalii, zikiwemo filamu za Tanzania - the Royal Tour na Amazing Tanzania ambazo zimeleta mafanikio makubwa kwa nchi.

"Mathalani, sote tumeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watalii nchini, ambapo kwa mwaka 2024, Tanzania imeweka rekodi ya kufikia watalii 5,360,247."

Dkt.Biteko amesema,kati ya hao 2,141,895 walikuwa wa kimataifa na 3,218,352 walikuwa watalii wa ndani.

Vilevile, kwa mwaka 2024 amesema,sekta ya utalii imeingiza mapato ya Dola za Marekani bilioni 3.9 na kuendelea kuzalisha fursa mbalimbali za ajira na uwekezaji kupitia mnyororo wake wa huduma.

Kwa upande mwingine, amesema Tanzania imeendelea kutambulika na kushinda tuzo mbalimbali ambazo pia ni chachu katika kuvutia watalii katika soko la kimataifa.

"Hatua hiyo imedhihirishwa kwa mafanikio ya kishindo kwa kupata Tuzo maarufu Duniani za World Travel Awards (WTA) zinazotolewa na taasisi ya World Luxury Media Group Limited ya nchini Uingereza katika msingi wa kutambua na kutangaza ubora wa vivutio vilivyopo."
Vivutio hivyo amesema ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro, kuwa mahali bora pa kutembelea barani Afrika kwa shughuli za utalii wa safari.

Sambamba na kupewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za World Travel Awards kwa Kanda ya Afrika zitakazotolewa mwezi Juni, 2025.

"Kwa kutambua mchango muhimu wa Onesho la KARIBU-KILIFAIR 2025 katika kuitangaza Tanzania, ninatoa pongezi na shukrani kwa Kampuni ya Karibu Fair Travel and Tourism kwa kuandaa kikamilifu onesho hili kwa kushirikiana na wizara zenye dhamana ya masuala ya utalii upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, bila kuwasahau Wafadhili na wadau wote washiriki kutoka upande wa Sekta ya Umma na Binafsi.

"Ushirikiano wenu mzuri, ni kielelezo kimojawapo cha utekelezaji kwa vitendo wa maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa Mzalendo na Muongoza Watalii Namba 1 katika kuitangaza Tanzania na kuendeleza sekta ya utalii nchini."
Mbali na hayo ameitaka wizara kuendelea kubuni njia mbalimbali za uendelezaji wa mazao ya utalii nchini kwa kuzingatia mgawanyiko wa aina ya mazao na mtawanyiko wa kijiografia wa nchi yetu.

Pia,kutumia fursa za ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika utangazaji utalii na upatikanaji wa masoko ya utalii.

"Na kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara za utalii nchini ili kuchochea na kuvutia uwekezaji zaidi.

"Aidha, kwa upande wa Sekta Binafsi natoa rai kwenu kuendelea kuwekeza katika sekta ya utalii, hususan katika eneo la huduma za malazi, ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya soko hasa tukizingatia uwepo wa matukio mbalimbali ya kimataifa yatakayofanyika nchini kadhalika na mwitikio chanya wa watalii kutoka katika masoko yetu ya kimkakati na yale yanayokua kwa kasi duniani.

"Niwahakikishie kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana nanyi wadau katika nyanja mbalimbali kuhakikisha ustawi wa biashara za utalii nchini na maendeleo ya sekta kwa ujumla wake."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news