Serikali imedhamiria kuibadili Pemba kuwa kitovu cha biashara na maendeleo jumuishi-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuifanya Pemba kuwa kitovu cha uwekezaji, biashara na maendeleo jumuishi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali imelenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje wenye mtazamo wa muda mrefu, ili kuleta maendeleo shirikishi, ajira kwa vijana na kuongeza pato la wananchi wa Pemba kwa uwekezaji wenye tija na endelevu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 16,2025 katika uzinduzi wa Tamasha la Uwekezaji Zanzibar 2025 linaloendelea katika Maeneo Huru ya Uwekezaji Maziwang’ombe Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa tamasha hilo ni mwanzo mzuri wa kuitangaza Pemba kitaifa na kimataifa, kwa kuonesha fursa na vivutio vilivyopo kisiwani humo, hususan katika sekta za uwekezaji, utalii, kilimo na viwanda vidogo.

Amebainisha kuwa Serikali imeweka vivutio maalum kwa wawekezaji watakaochagua kuwekeza Pemba ili kuwawezesha kufikia matarajio yao pamoja na kuinua hali za kiuchumi kwa wananchi wa Pemba.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeandaa sheria maalum inayowataka wawekezaji kutoa huduma za kijamii kwa wananchi waliomo katika maeneo ya uwekezaji ili wananchi wanufaike na miradi inayowekezwa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa tamasha hilo sasa litafanyika kila mwaka na kuthibitisha kuwa Tamasha lijalo la Zanzibar Investment Summit 2026 litafanyika Unguja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news