Serikali yapaisha huduma ya maji kwa wananchi

DAR-Nchi ya Tanzania ni moja kati ya nchi zilizopiga hatua kubwa katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza. 

Kwa juhudi za Serikali ikishirikiana na wananchi, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini imeimarika kwa kiwango kikubwa, kulingana na takwimu za Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 (Toleo la 2025).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhiwa tuzo ya kinara wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika huduma ya maji kwa jamii barani Afrika (The Panafrican Water, Sanitation and Hygiene Champion Award) kutoka taasisi inayojishughulisha na masuala ya maji ya WaterAid ya Uingereza wakati wa Siku ya Maji Maji Duniani 2025, jijini Dar es salaam.

Mapinduzi ya Sekta ya Maji yanahusisha utawala bora, uwajibikaji na ushirikishaji wa jamii kwa ujumla.

Kwa uchache Tanzania imeongoza na kuwa darasa la Dunia katika utekelezaji wa programu ya maji ya lipa kwa matokeo (p4r) kati ya nchi zaidi ya 50. Ni propgramu ambayo inasimamiwa na Beki ya Dunia (WB).

Mafanikio Vijijini

Katika maeneo ya vijijini, upatikanaji wa huduma za maji umeongezeka kutoka asilimia 50 ya mwaka 2002 hadi kufika asilimia 83 mwezi Juni 2024. Haya ni mafanikio makubwa yanayotokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miradi mipya ya maji pamoja na ukarabati na upanuzi wa miradi iliyopo.

Kulingana na Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 (Toleo la 2025), juhudi hizi zinahakikisha kwamba kila Mtanzania, bila kujali mahali alipo, anapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama.

Hadi mwezi Juni 2024, jumla ya miradi 2,943 ya maji ilikuwa imekamilika, ikiwa na vituo vya vya umma vya kuchota maji vipatavyo 169,515 na maunganisho ya nyumba 194,591.

Miradi mingi imejengwa kuhudumia zaidi ya kijiji kimoja na mingine hutumika kusafirisha maji hadi miji jirani na chanzo. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu Tanzania (2022), watu 34,950,360 kati ya 39,232,990 wanapata huduma ya maji vijijini.

Sera ya Maji inaelekeza kuwa kila kituo cha maji kihudumie wanufaika wasiozidi idadi ya 250 na kiwe ndani ya mita 400 kutoka katika makazi.

Hata hivyo, ieleweke kuwa ipo changamoto ambayo ni mahitaji kuongezeka kila kukicha ambayo hata hivyo Serikali inakabiliana nayo kwa kuangalia vyanzo vya maji vikubwa na miradi makubwa zaidi.

Kulingana na toleo jipya la Sera toleo la 2025, Serikali hivi sasa inaelekeza nguvu katika ujenzi wa miradi mikubwa inayotumia teknolojia ya kisasa inayoweza kuhudumia vijiji vingi kwa wakati mmoja.

Kwa kuwa miradi hiyo ni ya gharama kubwa, inapendekeza utaratibu wa kusaidia jamii uwezo zaidi katika kujua uwekezaji na uendeshaji wake.

Upanuzi wa Huduma Unavyoimarika Mijini

Kwa upande wa mijini, hali ya upatikanaji wa maji nayo imeimarika zaidi kutoka asilimia 73 mwaka 2002 hadi asilimia 91.6 mwaka 2024.

Hili ni kutokana na uwekezaji mkubwa katika kuboresha vyanzo vya maji, ujenzi wa mabwawa, mitambo ya kusafisha na kutibu maji, matenki ya kuhifadhi maji na mitandao ya usambazaji maji, kulingana na Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 (Toleo la 2025).

Kuanzia mwaka 2015 hadi 2024, mtandao wa usambazaji maji umeongezeka kutoka kilomita 8,662 hadi kilomita 27,534, na uwezo wa matenki ya kuhifadhi maji ukiongezeka kutoka mita za ujazo 712,933 hadi mita za ujazo 857,900. Majisafi yanapotumika, asilimia 80 huwa majitaka. Pichani ni moja ya mabwawa ya majitaka Mkoani Arusha ambapo huduma za kutolewa kwa serikali na sekta binafsi katika kuondosha majitaka katika makazi ya wananchi.

Sera inasisitiza ufanisi wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira katika kuongeza wigo wa huduma ili kuongeza mapato na kujitegemea zaidi kifedha, pamoja na kuimarusha huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, upatikanaji wa maji kwa wananchi unafanyiwa kazi na Serikali ili kuondosha changmoto za upotevu na mgao. 

Moja yah atua kubwa katika kuondosha hilo ni matumizi ya Dira za malipo kabla na kuwa na Gridi ya maji, ambayo itatoa maji katika maeneo ya maziwa na mito makubwa kupeleka katika maeneo yenye uhaba wa vyanzo, hivyo kuimarisha huduma yam aji kwa wananchi.

Pamoja na hilo Sera Toleo la 2025 imeweka msisitizo kwenye matumizi ya teknolojia na ufuatiliaji wa matumizi ya maji ili kudhibiti upotevu.

Matumizi Mengine ya Maji: Mwelekeo Mpya wa Sera

Toleo la Mwaka 2025 la Sera ya Maji linalenga si tu kwenye matumizi ya maji kwa nyumbani na mifugo, bali pia linaweka mkazo mkubwa kwenye mahitaji ya maji kwa sekta nyingine mtambuka na muhimu kwa uchumi na maendeleo ya wananchi ikiwamo kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda, migodi, huduma za mazingira na utalii.

Sera imeelekeza kuwepo kwa Mipango Jumuishi ya Matumizi ya Maji kati ya sekta mbalimbali ili kuondoa mgongano, kulinda mazingira na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za maji.

Huduma kwa taasisi za umma kama shule, masoko na vituo vya afya pia zimepewa kipaumbele katika sera hii.

Kwa mfano, hadi mwaka 2019, kupitia Mpango wa masuala ya maji (WASH), Serikali ilikuwa imesambaza maji kwenye idadi ya vituo vya afya vipatavyo 2,105 na shule 8,832 kati ya 19,995 zilikuwa na miundombinu ya huduma ya majisafi kupitia mabomba, visima au uvunaji wa maji ya mvua.

Kuhusu mifugo, Serikali ilijenga mabwawa 1,384, majosho 458 na visima virefu 103 hadi Juni 2024. 

Sera ya 2025 inasisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma hizi ili kupunguza uhamaji wa wafugaji, ambao huongeza migogoro ya ardhi na uchafuzi wa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mafanikio ya Tanzania katika kuimarisha huduma za maji ni ya kutia moyo. Lakini Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 (Toleo la 2025) inaweka msisitizo mkubwa zaidi kwenye matumizi jumuishi, usimamizi wa pamoja wa vyanzo vya maji, na matumizi ya teknolojia kuhakikisha huduma endelevu kwa wote.

Maji ni uhai siku zote, na sasa ni zaidi ya wakati mwingine wowote kutokana na maendeleo mbalimbali yanayoshuhudiwa Duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news