Wabunge wapewa semina kuhusu SEMA na BoT,kanuni mpya ya Matumizi ya Fedha za Kigeni

DODOMA-Wataalamu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha na Kurugenzi ya Masoko ya Fedha wamefanya semina kwa Kamati tatu za Bunge kuhusu mfumo mpya wa kusikiliza malalamiko ya wateja wa taasisi za fedha (SEMA na BoT) na Kanuni mpya ya Matumizi ya Fedha za Kigeni.
Semina hizo zimefanyika Jumatano Juni 11, 2025 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Ijumaa Juni 13, 2025 kwa Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) bungeni jijini Dodoma.

Msingi wa semina hizo ni kupokea maoni na kuwapa wabunge uelewa wa kina kuhusu namna Benki Kuu inavyoshughulikia malalamiko katika sekta za fedha, kuchochea ubunifu katika sekta hiyo pamoja na utekelezaji wa kanuni mpya za matumizi ya fedha za kigeni nchini.

Kuhusu namna ya kushughulikia malalamiko katika sekta ya fedha kwa taasisi zinazosimamiwa na BoT, Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha BoT, Bi. Violeth Luhanjo, alitoa wasilisho kuhusu mfumo mpya wa SEMA na BoT na namna unavyosaidia kukusanya na kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha.

Aidha, kuhusu Kanuni mpya za Matumizi ya Fedha za Kigeni nchini, wasilisho lilitolewa na Bw. Emmanuel Akaro ambaye ni Mkurugezi wa Masoko ya Fedha wa BoT, ambapo alifafanua mabadiliko yaliyofanywa, malengo yake, na namna kanuni hizo zinavyolenga kuimarisha uthabiti wa thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Kwa upande wake, Afisa Tehama kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha BoT, Bw. January Bura, alitoa wasilisho kuhusu namna Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha yatakavyosaidia kukuza ubunifu katika sekta hiyo.

Semina hizi zimetolewa ikiwa ni wiki moja tangu kuzinduliwa kwa mfumo wa kupokea malalamiko ya watumiaji katika sekta ya fedha wa SEMA na BoT na miezi michache tangu kupitishwa kwa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni 2025 nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news