Wachezaji Simba SC wapo tayari

DAR-Daktari wa Klabu ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam, Dkt.Edwin Kagabo amesema, wachezaji wote waliokuwa majeruhi wamerejea kikosini na wapo tayari kwa ajili ya mechi zilizopo mbele yao.
Dkt.Kagabo ameyasema hayo ikiwa ni siku mbili zimesalia kabla ya Simba SC kuvaana na Yanga SC katika mtanange wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Mtanange huo maarufu kama Derby ya Kariakoo inatarajiwa kupigwa Juni 15,2025 katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ingawa bado kuna mvutano unaochagizwa na kauli mbiu ya "Hatuchezi" kutoka kwa Yanga SC.

Aidha, amesema mlinda mlango Moussa Camara, walinzi Valentine Nouma na Che Fondoh Malone pamoja na kiungo Mzamiru Yassin ambao walikuwa majeruhi wamerejea na wanafanya mazoezi pamoja na wenzao.

"Maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mchezo wetu wa Jumapili na kikubwa zaidi ni kwamba kulikuwa na baadhi ya wachezaji ambao walikuwa na changamoto ndogo, kama mtakumbuka mchezo wetu wa Singida Black Stars wachezaji wetu wawili walipata changamoto.

"Kamara alipata changamoto ndogo ya kifua, ilikuwa na madhara yake,ameweza kurejea kwenye mazoezi na yuko timamu kabisa na amerudi katika mazoezi.

"Mchezaji mwingine Valentine Nouma ambaye alipata changamoto ya goti naye tumeshamuweka sawa na amesharudi kwenye mazoezi."

Kwa upande wa Che Fondoh Malone amesema, alikuwa na changamoto, lakini kwa sasa ameimarika na yupo tayari kwa mchezo.

"Pamoja na Mzamiru Yassin naye ameweza kurejea kwenye mazoezi kwa muda wote,kwa hiyo kwa ufupi ni kwamba tuna kikosi cha wachezaji wote ambao wapo tayari kwa mchezo."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news