Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yamtunuku tuzo ya heshima Rais Dkt.Mwinyi

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imemtunuku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi tuzo ya heshima kwa uongozi mahiri ambao umeendelea kuchagiza ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa kasi.
Tuzo hiyo imekabidhiwa na kupokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango leo Julai 30,2025 katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Uzinduzi huo umefanyika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam huku ukiongozwa na kaulimbiu ya "Tunaongoza Mustakabali wa Teknolojia katika Benki Kuu za Afrika".

Mfumo huo ambao ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wataalamu wa ndani wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na wataalamu wengine hapa nchini unatarajiwa kuwa na matokeo chanya katika sekta ya fedha nchini.

Katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Dkt.Mpango ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa ubunifu wa mifumo ya kidijitali ambayo amesema,ni hatua njema kwa ustawi wa sekta ya fedha nchini.

Akizungumzia kuhusu tuzo hiyo kwa Rais Dkt.Mwinyi, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Emmanuel Tutuba amesema kuwa, Rais Dkt.Mwinyi amekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi nchini.
"Mheshimiwa Makamu wa Rais, vilevile tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake mahiri na miongozo mbalimbali ambayo amekuwa akitupatia na kutuwezesha kutekeleza shughuli zetu, tumekuwa wanufaika sana na maelekezo yake ambayo yamekuwa yakituongezea tija na usahihi."

Pia, Gavana Tutuba amesema, wameshuhudia namna uchumi wa Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi unavyoimarika kwa kasi.

"Tumeshuhudia kwa namna mbalimbali kwa kadri ambavyo mazingira ya biashara Zanzibar yalivyoendelea kuboreshwa ikiwemo shughuli za uwekezaji na namna ambavyo idadi ya watalii imeongezeka na hata huduma za kibenki na miamala ya kidijitali imeongezeka ambayo yote haya yanachangia katika kuturahisishia kutekeleza majukumu yetu, sisi kama Benki Kuu na kukuza uchumi wa Taifa letu."

Amesema, mazingira ya ufanyaji biashara na shughuli za utalii Zanzibar zimeimarika zaidi,hivyo kuchagiza ongezeko la watalii visiwani humo ikiwemo ongezeko la miamala ambayo imewarahisishia BoT kutekeleza majukumu yake.

"Hivyo, hatuna cha kumlipa Dkt.Hussein Ali Mwinyi bali siku ya leo tumeandaa zawadi na tuzo ambayo nitaomba uipokee ili ikawe kumbukumbu katika uongozi wake."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news