Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yamtunuku Rais Dkt.Samia tuzo ya heshima kwa uchumi imara na himilivu

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imemtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan tuzo ya heshima kwa kuendelea kuufanya uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi,himilivu na imara.Tuzo hiyo imekabidhiwa na kupokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango leo Julai 30,2025 katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Uzinduzi huo umefanyika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam huku ukiongozwa na kaulimbiu ya "Tunaongoza Mustakabali wa Teknolojia katika Benki Kuu za Afrika".

Mfumo huo ambao ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wataalamu wa ndani wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na wataalamu wengine hapa nchini unatarajiwa kuwa na matokeo chanya katika sekta ya fedha nchini.
"Kipekee kabisa ninaomba kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti uliotuwezesha kutengeneza mfumo huu wa kimkakati."

Gavana Tutuba amesema, kwa ujumla Benki Kuu imekuwa ikitekeleza maelekezo mbalimbali ya Mheshiwa Rais Dkt.Samia ikiwemo ya kuhakikisha mifumo ya kielektroniki inasomana ili kuongeza tija na ufanisi katika huduma za Serikali zinazotolewa ndani na nje ya nchi.
Pia, amesema Benki Kuu imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Falsafa ya Mheshiwa Rais Dkt.Samia ya 4R inayowakilisha Maridhiano, Uthabiti, Mageuzi na Ujenzi Upya katika kushughulikia masuala ya sasa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.

"Ambayo imetusaidia sana kuongeza imani ya wananchi katika kutekeleza shughuli zao za kiuchumi katika kuboresha uwekezaji, kuimarisha mifumo ya malipo, kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza ukwasi katika mzunguko wa uchumi na kuimarisha thamani ya shilingi yetu ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni.

"Hivyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, hatuna cha kumlipa isipokuwa tumeandaa tuzo."
Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amemshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Isdor Mpango kwa kazi kubwa anayofanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais Dkt.Samia katika kutekeleza majukumu ya kila siku kwa ustawi bora wa jamii ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.

"Tunafurahi kukujulisha kuwa, katika kipindi chote cha Awamu ya Sita,uchumi wa Tanzania umeendelea kufanya vizuri kwa vigezo vyote vya Kitaifa na Kimataifa, licha ya changamoto mbalimbali zilizoukabili uchumi wa Dunia ikiwemo janga la UVIKO-19.

"Vita vya Ukraine na changamoto nyingine za mabadiliko ya tabianchi, kwa ujumla uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa kasi inayoongezeka kila mwaka kutoka asilimia 4.7 mwaka 2021 hadi asilimia 5.5 mwaka 2025."Gavana Tutuba amesema kuwa,kasi hiyo ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni kubwa ikilinganishwa na ukuaji wa uchumi wa Dunia wa asilimia 3.2 mwaka 2024.

"Ndiyo maana taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia, IMF, Moods na nyinginezo wamethibitisha uchumi wa Tanzania unakua vizuri, himilivu na imara."

Ameongeza kwamba, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika, thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika pamoja udhibiti wa mfumuko wa bei.
Gavana Tutuba amesema, hadi kufikia Juni, 2025 akiba ya fedha za kigeni ilifikia jumla ya dola za Marekani bilioni 6.2 ikiwa ni kiasi cha juu zaidi kufikiwa hapa nchini.

Wakati huo huo,Makamu wa Rais Dkt.Philip Isdor Mpango ameipongeza BoT pamoja na wataalamu wake waliotengeneza Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) wenye viwango vya kimataifa na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na bei za mifumo kama hiyo kwenye soko la kimataifa.
Dkt.Mpango amasema, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa taasisi ya kwanza barani Afrika kuunda Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki ambapo jumla ya shilingi bilioni 81.32 zimeokolewa kwa kutumia wataalam wa ndani na kuongeza ufanisi wa Benki Kuu katika kusimamia ufanyikaji wa miamala pasipo vizuizi.

Aidha, Gavana Tutuba amesema, mfumo wa iCBS umesaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuleta maboresho makubwa kwenye maeneo mengi ikiwemo utoaji wa taarifa sahihi za serikali na kwa wakati.

Vilevile utoaji wa taarifa za miamala, ufungaji wa hesabu kwenye akaunti za wateja, upatikanaji wa taarifa kwa wafadhili, uhaulishaji wa fedha na ukokotoaji wa riba za kibenki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news