DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepata ushindi wa pili katika kundi la Taasisi za Udhibiti katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yaliyofungwa rasmi Julai 13, 2025, na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).
Tuzo hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na kupokelewa na Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bw. Deogratias Mnyamani, kwa niaba ya Gavana Emmanuel Tutuba.
Ushindi huo ni uthibitisho wa jitihada thabiti na endelevu za Benki Kuu katika kuelimisha wananchi kuhusu majukumu yake pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu huduma za fedha.
Kupitia utoaji wa elimu hii, Benki Kuu inalenga kuwajengea wananchi uelewa wa kina kuhusu masuala ya uchumi na fedha ili waweze kushiriki kikamilifu katika mifumo rasmi ya kifedha na kufanya maamuzi sahihi yanayochangia ustawi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

