NA DIRAMAKINI
UONGOZI wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ambayo ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti umeonesha uungwana kwa kumuomba radhi aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ambaye kwa sasa ni Msajili wa Hazina, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu kutokana na tuhuma zilizowahi kuchapishwa katika Gazeti la The Citizen.
MCL wameomba radhi hiyo leo Julai 14,2025 kupitia magazeti yake katika kurasa za mbele huku wakikiri kuwa, makala hiyo ya mwaka 2018 ilikuwa na mapungufu ya kitaaluma.
"Kampuni ya Mwananchi Communications Limited,wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti inaomba radhi kwa Nehemiah Kyando Mchechu kutokana na makala iliyochapishwa katika toleo Na.4551 la Gazeti la The Citizen la Ijumaa ya Machi 23,2018.
"Tunakiri kuwa, habari hiyo ilikuwa na tuhuma ambazo imebainika za kudhalilisha dhidi ya Mchechu na ilikuwa na upungufu kitaaluma. Kwa sababu hiyo, tunaomba radhi kwa usumbufu, madhara na fedheha iliyosababishwa na taarifa hiyo,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo ya MCL.
Chanzo
Juni 4,2025 Mahakama ya Rufani Tanzania ilitupilia mbali maombi ya rufani namba 658 ya mwaka 2023 yaliofunguliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) ambayo ilimuhusisha Mhariri na Gazeti la The Citizen dhidi ya Nehemia Kyando Mchechu.
Mahakama hiyo ilikubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwenye kesi Namba 48 ya mwaka 2021 kati ya MCL kuhusu Mhariri na Gazeti la The Citizen dhidi ya Nehemia Kyando Mchechu uliosomwa Machi 3,2023 mbele ya Jaji Mgonya.
Katika uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani Tanzania uliotolewa na majaji watatu wa mahakama hiyo,Mheshimiwa Rehema Kerefu, Omar Othman Makungu na Dkt.Benhajj Masoud mahakama ilitupilia mbali hoja tatu za msingi.
Mosi kama Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo kusikiliza shauri hilo, pili kama mdai ambaye ni Nehemia Kyando Mchechu aliweza kuthibitisha madai yake ya kudhalilishwa.
Hoja ya tatu ni kama mahakama ilitumia utaratibu sahihi kutoa nafuu ambazo zilitolewa na Mahakama Kuu.
Aidha,majaji hao wa Mahakama ya Rufani walikubaliana na hoja za wakili wa utetezi wa mjibu maombi, Wakili Aliko Harry Mwamanenge na kuona kwamba Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kwamba mjibu rufani alifanikiwa kuthibitisha madai yake ya kudhalilishwa na pia Mahakama Kuu ilitumia utaratibu sahihi kufikia tuzo ambayo ilitoa.
Hivyo,Mahakama ya Rufani haikuona sababu ya kubatilisha au kubadilisha chochote kwenye maamuzi ya Mahakama Kuu na kuyabariki maamuzi hayo kama yalivyo.
Katika Mahakama Kuu, maamuzi yalikuwa ni Gazeti la The Citizen kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye kwa sasa ni Msajili wa Hazina, Nehemia Kyando Mchechu fidia ya shilingi bilioni 2.5 baada ya kuthibitika kuwa, taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo Machi 23, 2018 haikuwa na ukweli wowote.
Kupitia ukurasa wa mbele gazeti hilo liliandika habari iliyobeba kichwa cha habari, 'Kwa nini JPM alivunja Bodi ya NHC na kumng’oa Mchechu?' (Why JPM dissolved NHC Board, Sacked Mchechu).
Hukumu hiyo ya Kesi Na.48 ya 2021 ilitolewa Machi 3, 2023 na Jaji Leila Mgonya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Wakili wa Mchechu, Aliko Mwamanenge na Wakili wa Gazeti la The Citizen, Ambrose Nkwera.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mgonya alisema, katika adhabu hiyo,The Citizen wanapaswa kumlipa Mchechu shilingi bilioni mbili kama fidia kwa kumchafulia jina alilolijenga kwa muda mrefu huku shilingi milioni 500 zikiwa ni kwa ajili ya kumsababishia hasara ya jumla.
Jaji Mgonya alifafanua kuwa, pia gazeti hilo linapaswa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi ikiwemo kuandika habari ya kumuomba radhi Mchechu katika ukurasa wa mbele.
Alisema, radhi hiyo ilipaswa kuombwa kwa ukumbwa ule ule wa Machi 23, 2018 na watalipa riba ya asilimia 12 kila mwaka endapo watashindwa kulipa fedha hizo kwa wakati kuanzia Machi 3, 2023.
Pia,Mahakama hiyo ililionya Gazeti The Citizen na kulitaka kutomwandika tena Mchechu kwa habari za uongo na zenye kumchafulia jina kwa namna hiyo, isipokuwa tu pale ambapo wanakuwa na ushaidi na vielelezo vya kutosha kwa ajili ya habari.
Vile vile, Mahakama ilitoa nafasi ya upande wa mlalamikiwa kukata rufaa iwapo hajaridhika na maamuzi hayo.
Awali, Mchechu aliiomba Mahakama iamuru Gazeti la The Citizen kumlipa fidia ya shilingi bilioni tatu na kumwomba radhi, kwa madai ya kumchafulia jina na kushusha hadhi na heshima yake katika jamii.
Aidha,habari hiyo iliainisha sababu kadhaa kutoka vyanzo vyake mbalimbali, zinazodaiwa kuwa sababu za Rais wa Awamu ya Tano,Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, kuchukua uamuzi wa kuivunja Bodi ya NHC na kumuondoa Mchechu.
Jaji Mgonya alisema, baada ya wahariri wa gazeti la The Citizen kuwasilisha ushaidi na vielelezo vyao mahakamani hapo, havikuthibitisha tuhuma zilizoelekezwa kwa Mchechu kupitia habari hiyo, hivyo Mahakama haikubaini ukweli wowote.
Baadhi ya tuhuma zalizoibuliwa kwenye habari hiyo, ni pamoja na madai kwamba Mchechu alikuwa akichunguzwa na Bodi ya Wakurugenzi ya NHC na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu mgongano wa madaraka juu ya ununuzi wa ekari 500 za mradi wa NHC Safari City, Arusha.
Pia gazeti hilo lilidai kuwa Mchechu anachunguzwa na TAKUKURU kwa madai ya kumtumia mkandarasi aliyekodishwa na NHC, kujenga barabara yake binafsi karibu na mradi huo wa NHC Safari City.
Kuhusu mradi wa Kawe, gazeti hilo lilidai kuwa Mchechu aliingia makubaliano na kampuni ya ukandarasi ya PHILS International yenye makao yake Dubai, bila kushirikisha kitengo cha ununuzi wa NHC.
Hoja zingine zilizotajwa kwenye habari hiyo, ni kuhusu madai kwamba Mchechu anachunguzwa kwa tuhuma kuwa kampuni ya mkewe, ilipewa zabuni ya kutoa huduma za bima kwenye nyumba za NHC Mtwara, hali ambayo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Madai ya mwisho yaliyotajwa na gazeti hilo ni tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi yaliyotajwa kwa kiwango kikubwa.


