𝐓𝐅𝐒 𝐲𝐚𝐩𝐨𝐧𝐠𝐞𝐳𝐰𝐚 𝐤𝐰𝐚 𝐦𝐚𝐩𝐢𝐧𝐝𝐮𝐳𝐢 𝐦𝐚𝐤𝐮𝐛𝐰𝐚 𝐒𝐚𝐛𝐚𝐬𝐚𝐛𝐚

DAR-Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umepokea pongezi kubwa kwa kuonesha ubunifu na kufanya mapinduzi makubwa katika Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu.
Akitoa pongezi hizo leo, Julai 7, 2025, Mwenyekiti wa Banda la Maonesho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ernest Mwamaja, alisema TFS imevuka matarajio kwa kuboresha muonekano wa mabanda, bidhaa na elimu inayotolewa sambamba na ushirikiano na wadau wa uhifadhi.

“Itoshe kusema TFS mwaka huu wamefanya mapinduzi makubwa. Sijawahi kuona jambo kubwa kama hili, nawapongeza sana kwa ubunifu na maandalizi haya ya kiwango cha juu,” alisema Mwamaja mbele ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, aliyewasili leo asubuhi kwenye banda hilo.

Prof. Silayo aliwasili katika banda hilo tayari kwa kushiriki katika shughuli za siku ya kumi ya maonesho hayo, ambayo yamefikia kilele chake leo Sabasaba Day kwenye Ukumbi wa Ali Hassan Mwinyi Hall, Mbaruku Mwandoro Square.

Mwamaja alieleza kuwa licha ya taasisi moja pekee, Likuyu Sekamaganga, kushindwa kushiriki mwaka huu, taasisi zote za Wizara ya Maliasili na Utalii zimehudhuria kikamilifu na kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema banda la wizara limevunja rekodi kwa kuhudumia wageni 113,053 kwa siku moja pekee, wengi wao wakivutiwa na wanyamapori, duka la asali la TFS, shamba la nyuki lenye tiba maalumu ya kudungwa na nyuki, pamoja na ubunifu wa Mr Tree ambaye amegeuka kuwa kivutio maalumu kwa wageni.

Wananchi wengi wamekuwa wakijipatia kumbukumbu za kipekee kwa kupiga picha kwenye maeneo maalumu ndani ya banda la TFS, jambo lililodhihirisha ubunifu na umakini wa taasisi hiyo katika kuleta elimu ya uhifadhi kwa njia ya kuvutia.

Prof. Silayo amepongeza maandalizi hayo na kusisitiza kuwa TFS itaendelea kuboresha ubunifu na huduma ili maonesho ya mwaka ujao yawe makubwa zaidi na yenye manufaa kwa wizara nzima pamoja na wadau wote wa uhifadhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news