BoT Academy na WFP wafungua ukurasa mpya elimu ya fedha

NA GODFREY NNKO

CHUO cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ili kuwajengea uwezo wa elimu ya fedha vijana wanufaika wa Mradi wa Vijana Kilimo Biashara nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Julai 31,2025 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Emmanuel Tutuba.

Akizungumzia kuhusu makubaliano hayo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Emmanuel Tutuba amewapongeza WFP kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa, vijana wanufaika wa mradi huo wanakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu elimu ya fedha.

"Leo tumekutana kusaini na kukabidhiana rasmi Mradi wa Vijana Kilimo Biashara, mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa Chuo cha Benki Kuu (BoT Academy) kule Mwanza pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP). Wenzetu wa WFP wamekubali kufadhili masuala ya fedha ambayo yatatolewa kwa vijana mbalimbali katika mikoa saba hapa nchini."

Gavana Tutuba amesema, mradi huo utawawezesha vijana ambao wanapewa elimu ya masuala ya kifedha kuwa na uwezo wa kufanya shughuli zao za kilimo kwa kujikita zaidi kwenye uzalishaji bora na wenye tija kupitia kilimo cha mboga mboga,mtama pamoja na alizeti.

Pia, amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa, inashirikiana na wadau mbalimbali kama ilivyo kwa WFP ili kuhakikisha kuwa makundi yote ya kijamii ambayo hayajafikiwa na elimu ya fedha inawafikia.

Miongoni mwa makundi hayo, Gavana Tutuba amesema ni pamoja na wanawake, watu wenye ulemavu, wavuvi na wajasiriamali wadogo.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) hapa nchini, Christine Mendes amesema kuwa, Mradi wa Vijana Kilimo Biashara (VKB) unaotekelezwa na shirika hilo kwa ufadhili wa Mastercard Foundation umelenga kuwapatia vijana wakulima wadogo ujuzi na rasilimali zinazohitajika.

Amesema, lengo ni ili kuboresha uzalishaji wa chakula na kujenga uchumi endelevu ambapo mradi huo wa miaka mitano ulianza kutekelezwa mwaka 2022.

Bi.Mendes amesema kuwa,tangu mradi huo uanze umewafikia vijana 83,000 ambapo asilimia 70 ya vijana hao ni wanawake kutoka mikoa saba ukiwemo Manyara, Arusha, Dodoma, Singida, Tabora,Simiyu na Shinyanga.

Aidha, Bi.Mendes amesema kuwa, hadi kukamilika kwa kwa mradi huo mwaka 2027 wanatarajia kufikia lengo la kuwajengea uwezo vijana 115,000.

Kupitia ushirikiano huo ambao, WFP Tanzania itatoa ufadhili wa dola 100,000 (zaidi ya shilingi milioni 250), Bi.Mendes amesema, utawezesha wanufaika kupata uelewa wa masuala ya fedha kuhusu namna ya kusimamia fedha binafsi na ujuzi katika kujipangia bajeti, kuweka akiba, kuwekeza kwa ustawi bora kupitia shughuli zao za kilimo.

Amesema, kupitia makubaliano hayo na BoT Academy wanatarajia wanufaika wa Mradi wa Vijana Kilimo Biashara watapata uelewa wa kutosha ili kuwa na huru wa kifedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news