DCEA yabaini maiti,vitabu kutumika kusafirisha dawa za kulevya,maelfu ya tani yakamatwa

NA GODFREY NNKO

UWEKEZAJI unaofanywa na Serikali wa vifaa vya kisasa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) umeendelea kutoa matokeo chanya, baada ya watuhumiwa 64 kukamatwa na maelfu ya kilo za dawa za kulevya nchini.
Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo amethibitisha hayo leo Julai 9,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar Es Salaam.

Amesema,katika kipindi cha mwezi Mei hadi Julai, 2025 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na yombo vingine vya dola imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini na kukamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu 37,197.142.

Dawa hizo zinajumuisha, kilogramu 11,031.42 za dawa mpya za kulevya (New Psychoactive Substance) aina ya Mitragyna Speciosa, bangi kilogramu 24,873.56,mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, heroin kilogramu 2.21 na methamphetamine gramu 1.42.

Pia,Kamishna Jenerali Lyimo amesema ukamataji huo umehusisha dawa tiba zenye
asili ya kulevya aina ya ketamine kilogramu 1.92, Fluni-trazepam (rohypnol) vidonge 1000, lita 6 za kemikali bashirifu aina ya hydrochloric acid na uteketezaji wa ekari 1045.5 za mashamba ya bangi.

"Kadhalika, kilogramu 26 za dawa za kulevya aina ya heroin, zilizokuwa ziingizwe nchini kutokea nchini Msumbiji zilizuiwa na watuhumiwa 64 walikamatwa wakihusishwa na dawa hizo."

Katika operesheni iliyofanyika bandari kavu eneo la Temeke jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kiliogramu 11,031.42 za dawa za kulevya aina ya Mitragyna speciosa zilizoingizwa nchini kutokea nchini Sri Lanka zilikamatwa zikiwa kwenye vifungashio vyenye chapa inayoonesha kuwa ndani yake kuna mbolea.

"Mitragyna speciosa iko katika kundi la dawa mpya za kulevya zinazotokana na mimea inayofahamika kwa jina la Kratom.Mmea huu una kemikali aina ya Mitragynine na 7-Hydroxymitragynine (7-HMG) ambayo inasifa ya vichangamshi na vipumbaza vyenye madhara ya kiafya kwa mtumiaji, kwani huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu hata kupelekea vifo vya ghafla."
Katika operesheni iliyofanyika eneo la Posta jijini Dar es Salaam, watuhumiwa sita, wakiwemo raia wawili wa China wanaofahamika kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin walikamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine gramu 1.42, dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya frunitrazepam (rohypnol) vidonge 1,000 na Ketamine zenye uzito wa Kilogramu 1.92.(Picha na DCEA).

Vilevile amesema, katika operesheni iliyofanyika eneo la Posta jijini Dar es Salaam, watuhumiwa sita wakiwemo raia wawili wa China wanaofahamika kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin walikamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine gramu
1.42.

Pia,walikuwa na dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya frunitrazepam (rohypnol) vidonge 1,000 na Ketamine zenye uzito wa Kilogramu 1.92.

"Mkoani Dar es Salaam eneo la Sinza walikamatwa watu wawili wamiliki wa kiwanda bubu kinachotengeneza biskuti zinazochanganywa na bangi kisha kuzisambaza katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara."
Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mkoani Lindi alikamatwa mfanyabiashara wa madini akisambaza biskuti zilizochanganywa na bangi.

Kwa upande wa dawa za kulevya za mashambani, zilikamatwa jumla ya kilogramu
26,191.45 za bangi, mirungi, skanka na kuteketeza ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora,Morogoro na Arusha.

Amesema,mamlaka imebaini kuwa, baadhi ya wahalifu wa dawa za kulevya wameanza tena kutumia maiti za binadamu kubeba dawa za kulevya, maarufu kwa jina la begi.

Aidha, kumekuwa na matukio ya raia wa kigeni kuwatumia watanzania kusafirisha au kusambaza dawa za kulevya.

"Mara nyingi, huanzisha mahusiano ya kirafiki na kisha kuwahusisha katika biashara hii haramu kwa kutumia kampuni zao na vyombo
vyao vya usafiri hususani bodaboda, bajaji, Tax na wasambazaji wa vifurushi.

"Hivyo basi, wananchi wanapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari kubwa hasa pale wanapotumwa au kupokea mizigo kutoka kwa watu wasiowafahamu vyema.

"Ni muhimu wajiridhishe na mizigo wanayoisafirisha ili kuepuka kujikuta wakihusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya.
Katika operesheni iliyofanyika bandari kavu eneo la Temeke jijini Dar es Salaam, kilogramu 11,031.42 za dawa za kulevya aina ya Mitragyna speciosa zilizoingizwa nchini kutokea nchini Sri Lanka zilikamatwa zikiwa kwenye vifungashio vyenye chapa inayoonesha kuwa ndani yake kuna mbolea. (Picha na DCEA).

"Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa kuwafichua watu wanaojihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ili tatizo la dawa za kulevya litabaki historia hapa nchini.

"Hata hivyo,kwa yoyote atakayejihusisha na uzalishaji, usambazaji na biashara ya dawa za kulevya,hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,"amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news