Dkt.Mpango azindua Makumbusho na Maktaba ya Kidijitali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT)

NA GODFREY NNKO 

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango amefungua rasmi Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania yenye lengo la kuonesha historia na maendeleo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Emmanuel Tutuba wakati akitembelea Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania yenye lengo la kuonesha historia na maendeleo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mara baada ya ufunguzi wa makumbusho hiyo uliofanyika katika ofisi za makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam tarehe 30 Julai 2025.

Sambamba na Maktaba ya Kidijitali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo itawezesha usomaji wa vitabu na majarida kwa njia ya mtandao.

Ufunguzi huo ambao umefanyika Julai 30,2025 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam umeenda sambamba na uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) wa BoT.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifungua rasmi Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania yenye lengo la kuonesha historia na maendeleo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Ufunguzi huo umefanyika wakati wa uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliyofanyika katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kuhusu uzinduzi huo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Emmanuel Tutuba amemshukuru Makamu wa Rais Dkt.Philip Isdor Mpango kwa kukubali kuungana nao katika hafla hiyo muhimu kwa BoT.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais, tunakushukuru kwa kutuzindulia Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Maktaba ya Kidijitali ya Benki Kuu ya Tanzania, tuliona ni muhimu na busara kipindi cha sasa kuanzisha utaratibu wa kutunza kumbukumbu ya historia, chimbuko na mwenendo na shughuli mbalimbali za Benki Kuu ya Tanzania ili kuwa na kumbukumbu sahihi na zilizo rasmi kwa ajili ya jamii iliyopo, shughuli mbalimbali na hata kufanya rejea kwa vizazi vijavyo."
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Maktaba Kidijitali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliofanyika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam.

Pia, Gavana Tutuba amesema, waliamua kuanzisha Maktaba ya Kidijitali ili kutumia fursa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na urahisi wa upatikanaji wa taarifa kwa mafundisho, elimu, maarifa na mifano.

Vilevile kufanya rejea na stadi bobevu kwa wakati kutokana na watafiti, wanazuoni, waandishi na wachapishaji mahiri ambao wanatarajia kuunganishwa kwenye maktaba hiyo ambao watakidhi mahitaji ya wasomaji zaidi ya milioni 10 ambao watakuwa wanajisomea popote walipo duniani.

Katika hatua nyingine,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amewapongeza wataalam wa ndani katika kuubuni na kuuendesha mfumo huo wa iCBS.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) katika hafla iliyofanyika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Hafla hiyo imefanyika Julai 30,2025 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam.

Dkt.Mpango amesema,uundwaji wa mfumo huo kwa kutumia rasilimali watu wa ndani si tu mafanikio ya kiteknolojia, bali ni ushahidi wa uhuru wa kidijitali uliopatikana nchini.

Amesema,mafanikio hayo ni tofauti na kipindi cha nyuma ambacho kilitawaliwa na utegemezi kwa watoa huduma wa kigeni kuja kubuni na kuendesha mifumo ya namna hiyo.

Pia, amesema, huo ni ushindi tosha kwa upande wa kulinda taarifa za fedha nchini,hivyo mfumo huo ulindwe kama kila mmoja anavyothamini mboni ya jicho lake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news