DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, ameongoza kikao cha 12 cha Kamati hiyo kilichofanyika tarehe 9 Julai, 2025 katika Ofisi ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kinachohusisha mamlaka za Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha zipatazo 15 kimejadili masuala mbalimbali kuhusu Ripoti ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha Tanzania ya Mwaka 2024.Kamati hiyo inashughulika na masuala mbalimbali ya kustawisha sekta ya fedha yakiwemo kuimarisha usimamizi na kupunguza vihatarashi katika mfumo wa kifedha, mifumo ya usimamizi wa majanga katika sekta ya fedha, ushirikiano baina ya mamlaka za udhibiti wa sekta ya fedha na kuimarisha uwezo wa kifedha kwa watoa huduma za kifedha.








