NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kushusha Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) katika robo ya tatu ya mwaka kwa asilimia 5.75 kutoka asilimia 6 iliyodumu kwa robo mbili za mwaka 2025,ikiwa ni mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Emmanuel Tutuba ameyabainisha hayo leo Julai 3,2025 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Riba ya Benki Kuu, baada ya kamati hiyo kukutana Julai 2,2025. Riba hiyo itatumika kuanzia Julai hadi Septemba,mwaka huu.
Hatua hii,pia ni kiashiria kimojawapo katika upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza kutekeleza mfumo huu Januari,2024 badala ya mfumo uliokuwa unatumia ujazi wa fedha.
Kupitia mfumo huu, Benki Kuu ya Tanzania huwa inatoa mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki.
Lengo la Riba ya Benki Kuu ni kuwezesha ukwasi katika uchumi ili uendane na malengo ya kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa uchumi.
