GCLA yaongeza kasi utoaji matokeo ya uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imesema kuwa, imeongeza kasi ya utoaji matokeo ya uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba,ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali ili kuwezesha maeneo mengine ya kichunguzi kuendelea nchini.
Mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa upande wa vifaa vya kisasa hususani katika maabara ya teknolojia ya vinasaba.

Dkt.Fidelice Mafumiko ambaye ni Mkemia Mkuu wa Serikali ameyasema hayo leo Julai 10,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

GCLA ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya Mwaka 2016.

Aidha,pamoja na majukumu mengine, sheria ya mamlaka inaipa jukumu mamlaka ya kuwa chombo cha juu na Maabara ya Rufaa katika masuala yote yanayohusu uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba,ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali.

Dkt.Mafumiko amesema kuwa, lengo la mamlaka ni kuchangia katika kuimarisha ustawi wa jamii katika masuala ya afya na kulinda mazingira.

Amefafanua kuwa,uwekezaji huo umewezesha ongezeko la thamani ya mitambo kutoka shilingi bilioni 13.6 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi shilingi bilioni 17.8 mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.6.
Mkemia Mkuu wa Serikali amesema,kiasi hicho cha fedha kimetumika kununua mitambo mikubwa 16 na midogo 274, hatua iliyosaidia kuboresha ufanisi wa uchunguzi wa kimaabara kwa wananchi kote nchini.

Pia, amesema wanatarajia kuendelea kununua mitambo ya kisasa zaidi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora zaidi kwa umma.

Vilevile amesema,katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita mamlaka hiyo imefanikiwa kuongeza wadau waliosajiliwa kutoka 2,125 mwaka 2021 hadi kufikia 3,835 Juni 2025 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 81.

Pia,Dkt.Mafumiko amesema,mamlaka hiyo imekagua maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali ikiwa ni asilimia 119 ya lengo la ukaguzi wa maghala 7,160 na vibali vya kuingiza kemikali vimeongezeka kutoka 40,270 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 67,200 mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 40.

Katika hatua nyingine,mamlaka hiyo imechangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini hasa zile zinazotumika katika sekta ya madini.

Mkemia Mkuu wa Serikali amesema kuwa, matumizi ya kemikali muhimu yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka minne kwani Ammonium Nitrate tani 135,445 mwaka 2021/2022 imeongezeka hadi tani 461,777.42 mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 241.
Mkemia Mkuu wa Serikali amesema,Salfa imeongezeka kutoka tani 396,982 mwaka 2021/2022 hadi tani 1,867,104.72 mwaka 2025 ikiwa ni ngezeko la asilimia 370.32.

Aidha,Sodium Cyanide imeongeza kutoka tani 41,461 mwaka 2021/2022 hadi tani 63,103.4 mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 52.20.

Dkt.Mafumiko amesema, asilimia 80 ya shehena ya Ammonium Nitrate huingia kupitia Bandari ya Tanga, jambo linaloonyesha mafanikio ya uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya bandari hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kossuri amesema, vikao hivi endelevu vinalenga kuimarisha mahusiano baina ya vyombo vya habari na taasisi za umma ili ziweze kuelezea mafanikio na mikakati mbalimbali waliyonayo kwa umma.

Ikumbukwe kuwa,Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepitia mabadiliko mbalimbali kutoka kuwa idara ndani ya wizara,wakala kati ya mwaka 1999-2016 na kuwa mamlaka kuanzia Aprili 5,2017 hadi sasa.

Kihistoria mamlaka ilianza kama kituo cha kufanya utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto kwenye maabara ya taifa mwaka wa 1895 na baadae kuhamishiwa Wizara ya Afya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1947.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news