MORONI-Kikosi cha Wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania kimewasili nchini Comoro ambapo kinatarajiwa kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa nchi hiyo yatakayohudhuriwa pia na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan atakayekuwa Mgeni Rasmi.
Kikosi hicho kikiongozwa na Captain Mohammed Maulid Nchimba kimetembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro na kukutana na Balozi Saidi Yakubu pamoja na Mwambata Jeshi Kanali Abdulrahim Mahmoud Abdallah ambaye anaratibu ziara hiyo.
Akizungumza na askari hao Balozi Saidi Yakubu aliushukuru uongozi wa JWTZ hususan Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob John Nkunda kwa kukubali mwaliko wa Jeshi la Comoro na kutuma kikosi chake kunogesha maadhimisho hayo. Mbali na Tanzania, wanajeshi toka China na Morocco nao pia watashiriki.
Balozi Yakubu pia alieleza kuwa, ushiriki wa JWTZ katika maadhimisho hayo ni kielelezo cha ushirikiano wa hali ya juu wa majeshi ya nchi hizo mbili na kuwaeleza kuwa mara zote vikosi vya JWTZ wamekuwa ni kivutio kikubwa wanaposhiriki na hivyo mwaka huu ni matarajio ya wacomoro kuws hali hiyo itaendelea na kuwaeleza pia makundi mengine yanayoshiriki toka Tanzania yallyoalikwa ikiwemo vikundi vya burudani na mabondia.