DAR-Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ametoa rai kwa taasisi za fedha kuja na programu maalumu za elimu ya fedha kwa wasanii na wanamichezo. 

Mhe. Mwinjuma ametoa rai hiyo Julai 4,2025 jijini Dar es salaam wakati akizindua msimu wa tatu wa programu ya utoaji elimu ya fedha inayoendeshwa na Benki ya CRDB ijulikanayo kama zogo Mchongo.
Mhe. Mwinjuma amesema kundi hilo mara nyingi hujikuta lina kipato kikubwa kwa kipindi kifupi, lakini bila elimu ya fedha, maisha yao ya baadaye huwa magumu.
Naibu Waziri ameongeza kuwa elimu ya fedha ikiimarishwa, wananchi wataweza kutumia huduma za mikopo, kuwekeza kwenye masoko ya mitaji na dhamana maeneo ambayo bado ushiriki ni mdogo.
Naye Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Labala, amesema suala la elimu ya fedha sio la Serikali pekee bali linahusisha wadau wote wa maendeleo nchini hususan wao walioko katika sekta ya fedha ndiyo maana wameendeleza jitihada zaidi katika kutoa elimu ya fedha.
Amesema, msimu wa tatu wa programu hiyo utakuwa na maboresho makubwa ikiwemo kuongeza vipindi, kuboresha maudhui na kuongeza wataalam ambao wanahusika kujadili mada ili kuongeza mvuto katika uchangiaji wa mada.











