Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Law School waingia makubaliano ya kihistoria nchini

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School) wamesaini hati ya makubaliano (MoU) kwa ajili ya kufanya kazi kwa pamoja.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo Julai 2,2025 katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam,Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Mheshimiwa Hamza Johari amesema kuwa,lengo la makubaliano hayo ni kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo mafunzo.

"Kama mnavyofahamu taasisi hii ya Law School, ndiyo yenye dhamana ya mafunzo ya sheria kwa vitendo na ni taasisi ambayo imefanya kazi kubwa na nzuri katika Taifa letu."

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema, Law School ni taasisi ambayo ina uwezo thabiti huku ikiwa imejijengea heshima na imani kubwa kwa Taifa.

"Kwa hiyo sisi tuliona tusikae mbali na taasisi hii na tutafute namna ya kujenga mahusiano ya karibu na taasisi hii.

"Moja ya namna ya kujenga mahusiano ni hati za makubaliano ambazo zitaainisha maeneo mbalimbali ambayo tunadhani tunaweza kushirikiana."

Amesema, kupitia MoU ya leo itawezesha pande zote kushirikiana ikiwemo eneo la huduma za msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Johari amesema, eneo hilo bado ni changamoto hapa nchini, hivyo wameona wao kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni vema wakaliimarisha.

Lengo likiwa ni kuongeza ufanisi zaidi hususani kupitia vituo vya msaada wa kisheria ambavyo watavianzisha ikiwemo kamati za sheria za mikoa na wilaya kuwajengea uwezo wahitimu wa sheria.

Naibu

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli M. Maneno amesema, lengo la kusaini makubaliano hayo ni kwa ajili ya kuimarisha mahusiano kwa ajili ya sheria,huduma za kisheria na kuwajengea uwezo wataalamu wa sheria wanaozalishwa.

LST

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), Prof.Sist Mramba amesema,

"Tukio lililotukutanisha leo hapa ni tukio kubwa sana, ni tukio la kihistoria, ni tukio ambalo linatupa hatua nyingine katika utekelezaji wa majukumu yetu kama taasisi ya umma ambayo jukumu lake ni kuandaa wataalamu katika sekta ya sheria.Wataalamu ambao wamefunzwa kutekeleza sheria kwa vitendo."

Prof.Mramba mbali ya kuipongeza Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali kwa htua hiyo muhimu amesema,yaliyomo ndani ya hati hiyo ni mambo kwa ajili ya utekelezaji.

"Lakini,kama taasisi ya wanasheria kwa vitendo,tumefarijika na tutoe uhakika kwamba hati hii tuna uwezo wa kuitekeleza na majukumu yaliyoainishwa kwa sababu tumekuwa tukiandaa vijana au wanasheria kwa vitendo."

Amesema, kama sehemu ya kuwaandaa wanasheria kwa vitendo ni pamoja na namna ya kutoa msaada wa kisheria.

Pia,amesema wengi wamefanya hivyo katika maeneo mbalimbali na wana uzoefu wa kutosha.

"Kama taasisi pia, tumeshiriki katika kampeni ya Mama Samia Legal Aid kwenye maeneo mbalimbali nchini mbayo ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

"Kwa hiyo, hati hii inatupa hatua nyingine, moja kwa ajili ya kushiriki kwa karibu zaidi zoezi utoaji wa msaada wa kisheria na kuwapa wanafunzi wetu fursa kwa sababu kwa wanasheria zoezi la kujifunza,kujinoa ni zoezi endelevu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news