NA GODFREY NNKO
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imetoa rai kwa wananchi kutembelea banda lake lililopo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam ili kujifunza zaidi kuhusu namna mfumo wa bima ya amana unavyofanya kazi na nafasi yake katika kulinda akiba za wateja nchini.
Rai hiyo imetolewa leo Julai 2,2025 na Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw.Isack Kihwili wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo.
"Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Bodi ya Bima ya Amana kuwa na banda lake kwenye maonesho haya, tumezoea kuona miaka iliyopita tulikuwa tukishiriki maonesho haya tukiwa ndani ya banda la Benki Kuu ya Tanzania na sababu kubwa kwa muda mrefu Bodi ya Bima ya Amana imekuwa ikiendesha shughuli zake kama sehemu ya Benki Kuu ya Tanzania kama Kurugenzi.
"Lakini kuanzia sasa na kuendelea mchakato upo katika hatua nzuri wa kuifanya Bodi ya Bima ya Amana ijiendeshe yenyewe.
"Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwajulisha wananchi kuwa Bodi ya Bima ya Amana inasimama yenyewe, ninadhani itaweza kujielekeza vizuri katika kutekeleza majukumu yake na itapata nafasi nzuri pia ya kuwasiliana na wananchi bila kupitia Benki Kuu ya Tanzania
"Mwananchi yeyote ambaye ana amana kwa maana ya deposit katika benki au taasisi ya fedha iliyo na leseni ya Benki Kuu ya Tanzania,huyo ni mteja wetu kwa maana kwamba amana yake inalindwa na Bodi ya Bima ya Amana.
“Hivyo,tunahimiza watu kupata elimu sahihi. Kujua usalama wa fedha zako kunakusaidia kufanya maamuzi bora ya kibenki,” aliongeza.
Kuhusu tofauti iliyopo kati ya bima ya amana na bima nyingine,Kihwili amesema,katika bima za kawaida muhusika mbaye ni mteja huwa analipa kiwango fulani cha bima, lakini upande wa bima ya amana huwa hakuna ulipaji huo.
Amesema,hadi mwishoni mwa mwaka jana Mfuko wa Bima ya Amana ulikuwa na shilingi trilioni 1.04 ambazo zimetokana na mchango wa Serikali wa shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa wakati wa kuanzishwa mfuko huo mwaka 1994.
Pia,amesema kiasi hicho kinatokana na michango ya kila mwaka kutoka kwa wanachama ambao ni benki na taasisi za fedha na faida inayotokana na uwekezaji katika dhamana za Serikali.
DIB ina jukumu la kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana (DIF). DIF hupata fedha zake kutokana na vyanzo vikuu viwili, yaani michango kutoka benki na taasisi za fedha zinazopokea amana na mapato ya riba kutokana na uwekezaji.
Kwa kiasi kikubwa, rasilimali hizo huwekezwa katika dhamana zilizo chini ya udhamini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani Dhamana za Serikali na Hati fungani.
Uwekezaji hutegemea muda wa kuiva kulingana na masharti yaliyowekwa katika Sera ya Uwekezaji ya DIB.
Fidia
Wakati huo huo, Kihwili amesema,bodi hiyo imelipa fidia ya shilingi bilioni 9.07 kwa wateja wa benki saba zilizofungwa kutokana na kufilisika, hatua inayolenga kurejesha imani ya umma katika sekta ya fedha nchini.
Amesema,fidia hiyo inawakilisha asilimia 75.76 ya madai yote yaliyowasilishwa na wateja wanaostahili kufikia Machi,2025 huku asilimia iliyobaki ikiwa ni wateja ambao hawajawasilisha madai.
Kihwili amesema, malipo hayo yalifanyika kwa wateja wa EFATHA Bank Limited, FBME Bank Limited, Covenant Bank for Women (T) Limited, Kagera Farmers' Cooperative Bank Limited, Meru Community Bank Limited na Njombe Community Bank Limited.
Mkurugenzi huyo amewahimiza wateja wa benki zilizofungwa kutembelea ofisi za Bodi ya Bima ya Amana au kuwasiliana na wawakilishi wao ili kuwasilisha madai na kupata malipo yao.
Benki ya FBME ilichukua zaidi ya asilimia 57 ya madai yaliyolipwa, huku Covenant Bank ikiwa na asilimia 83.73, Benki ya Kagera asilimia 94.06, Benki ya Meru asilimia 92.35, Benki ya Mbinga asilimia 84.66, Benki ya Njombe asilimia 87.26, na Benki ya Efatha ikiwa sehemu ya waliolipwa.
“Kwa sasa tuna taasisi 42 (za kibenki) zinazochangia na zote zimesajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania. Kila benki huchangia asilimia 0.15 ya amana zake kwa mwaka kwenye mfuko huu,” alisema Bw. Kihwili.
Kiwango cha juu cha bima ya amana kwa mteja mmoja pia kimeongezeka kwa kipindi cha miaka. Kianzia shilingi 250,000 mwanzoni, kiwango hicho kilipandishwa hadi shilingi milioni 1.5 mwaka 2010, na kimefikia shilingi milioni 7.5 mwaka 2023.
“Hii inamaanisha kuwa endapo benki itafilisika leo, mteja yeyote mwenye hadi shilingi milioni 7.5 atalipwa fidia kamili. Kwa kiasi kinachozidi hapo, DIB hufuata taratibu za ufilisi na urejeshaji kwa kushirikiana na mamlaka nyingine,” alieleza Bw. Kihwili.
Bodi ya Bima ya Amana Tanzania imeanzishwa kwa dhumuni kuu la kuwalinda wenye amana wadogo kutokana na athari ya kupoteza amana zao pale benki au taasisi ya fedha inapofilisika.
Mkurugenzi huyo amesema, kufanya hivyo kunaufanya umma kuwa na imani na mfumo wa fedha nchini. Aidha,bodi hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 1991.
Kufuatia kufutwa kwa sheria hiyo,Bodi ya Bima ya Amana imeendelea kuwepo na kufanya kazi zake kwa mujibu wa kifungu cha 36 hadi 42 cha Sheria ya Mwaka 2006.
Pia,amesema bodi hiyo ipo katika mchakato wa kuboresha muundo wake kisheria na kiutendaji ili ichangie kikamilifu na kwa ubora zaidi katika uimarishaji wa mfumo wa fedha hapa nchini.
Amesema, mchakato huo unalenga kuifanya Bodi ya Bima ya Amana ijitegemee kisheria na kiutendaji kutoka chni ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tangu ianze majukumu yake mwaka 1994. Bodi ina wajibu wa kutunga sera, kusimamia na kudhibiti Mfuko wa Bima ya Amana nchini.
