NJOMBE-Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 19.6 kwa ajili ya Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) mkoani Njombe.
Kati ya fedha hizo jumla ya shilingi bilioni 4.360 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo majengo ya madarasa, maabara, mabweni,bwalo la chakula,jengo la utawala na nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Njombe ambayo imekamilika.Hayo yamebainishwa Julai 17, 2025 na Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Njombe,Mwalimu Nelasi Mulungu ambapo amesema,pia shilingi bilioni 1.6 imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Mkoa ya Amali ambayo inaendelea na ujenzi katika Wilaya ya Ludewa.
Mwalimu Mulungu amesema kuwa,Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 12.638 kwa ajili ya ujenzi wa shule 20 za kata katika mkoa huo wa Njombe.
Pia,amesema kuwa serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mingine katika mkoa wa Njombe ikiwemo ujenzi wa Mabweni, Nyumba za walimu na matundu ya vyoo.

