NA GODFREY NNKO
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yameendelea kumuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza na kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.
Rais Dkt.Samia ndiye kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ndani na nje ya Afrika ambapo hapa nchini inatarajiwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia kama inavyoelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.
REA na STAMICO ambazo ni taasisi za umma leo Julai 22,2025 jijini Dar es Salaam ili kuongeza kasi na ufanisi zimesaini mkataba wenye lengo la kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.58.
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse huku kwa pamoja wakithibitisha hiyo ni hatua muhimu katika kufanikisha ajenda ya nishati safi nchini.
"Wakala wa Nishati utatoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuanzisha kiwanda au mtambo wa kuzalisha mkaa mbadala unaoitwa rafiki katika Mkoa wa Geita,"amesema Mhandisi Saidy.
Wakati REA ikitoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kufanikisha mradi huo upande wa kununua mtambo, STAMICO itachangia shilingi bilioni 1.58 kwa ajili ya upatikanaji wa kiwanja,ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji mtambo.
Mhandisi Saidy amesema,utiaji saini wa mkataba huo kati ya REA na STAMICO ni moja wapo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wakala kushirikiana na STAMICO kuona namna ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi ili waondokane na matumizi ya nishati zisizo safi na salama.
“Ni matumaini yetu kuwa mkataba huu utaenda kuongeza kasi ya upatikaji wa mkaa mbadala na kwa bei nafuu ikiwa ni mojawapo ya lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia.
"Tunatambua kuwa utunzaji wa mtambo huu ni muhimu sana ili huduma iliyokusudiwa iendelee kutolewa kwa wakati bila kuathiri uchumi wa wananchi, afya pamoja na mazingira kwa ujumla."
Aidha,Mhandisi Saidy ameipongeza STAMICO kwa ajenda waliyoianzisha ambayo inalenga kuunga mkono Ajenda ya Taifa ya Nishati Safi ili kuhakikisha Watanzania wanahama kutoka nishati ambazo si salama kwa afya zao na mazingira.
Pia amesema, hatua hii ni muhimu katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan za kutekeleza Mpango wa Nishati Safi kwa ustawi bora wa mazingira na afya.
"Kwa hiyo, leo tumefungua ukurasa mpya kati yetu na wenzetu STAMICO,"amesema Mhandisi Saidy huku akibainisha kuwa, STAMICO imekuja na teknolojia ya kisasa ya kuboresha makaa ya mawe ili yaweze kutumika kama nishati safi na salama ya kupikia.STAMICO
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse amesema kuwa,mkataba huo utaifanya STAMICO kuwa na mitambo mikubwa mitano ya kuzalisha mkaa mbadala nchini.
Amesema,uzalishaji wa nishati hiyo ni endelevu kwani malighafi ambayo inatumika katika uzalishaji inapatikana kwa wingi huko Kiwira.
Dkt.Mwasse amesema,shirika hilo lilifanya utafiti wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kiwira ambapo tani milioni 300 za makaa ya mawe ziligundulika na zinaweza kutumika miaka 100 ijayo.
Vilevile amevitaja viwanda ambavyo vinaendelea na uzalishaji kuwa ni kilichopo Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani. Pia, kuna kiwanda kingine Kiwira Mkoa wa Songwe,Dodoma na Tabora ambavyo vipo katika hatua za ukamilishaji ili vianze uzalishaji.

Dkt.Mwasse amesema, wanatarajia kusimika kiwanda kingine mkoani Tanga ili kuhakikisha Watanzania wanafikiwa na nishati safi ya mkaa rafiki.
"Nishati hii itaendelea kupatikana kwa kadri itakavyokuwa inahitajika na itakuwa nafuu."



