Riba ya Benki Kuu (CBR) yashuka hadi asilimia 5.75, Gavana Tutuba ataka elimu ya fedha kusambaa vijijini

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Emmanuel Tutuba amezihimiza benki na taasisi za fedha zilizopo nchini kujiwekea utaratibu wa kufikisha elimu ya fedha kwa wananchi vijijini ili iweze kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Amesema, elimu hiyo licha ya kuwawezesha wananchi kufikia malengo yao ya kifedha, pia itawasaidia kuboresha ustawi wao na kujenga maisha wanayoyataka kiuchumi.
Gavana Tutuba ametoa rai hiyo leo Julai 3, 2025 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya tatu ya mwaka 2025 ambayo ni asilimia 5.75.

Riba hiyo imeshuka kutoka asilimia 6 ambayo ilidumu kwa robo mbili mfululizo na itadumu kuanzia Julai hadi Septemba, mwaka huu kabla ya Oktoba kutangazwa riba nyingine.

Katika mkutano huo ambao umewaleta pamoja viongozi wa benki na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania, Bw.Theobald Sabi amesema kuwa, kupungua kwa Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 6 ya robo iliyoisha hadi asilimia 5.75 kunaweza kuchangia kupunguza viwango vya riba vinavyotozwa na benki za biashara nchini.

Sabi ameweka wazi kuwa,viwango hivyo huathiriwa pia na vigezo vingine kama vile nguvu za soko na tathmini ya vihatarishi inayofanywa kwa mteja kabla ya kumpa mkopo.

Vilevile, Gavana Tutuba amesema, elimu ya fedha itawasaidia wananchi ambao wengi wamekaa na fedha zao nyumbani bila kuzipeleka benki, hivyo kufungua akaunti ili kuzipa usalama fedha zao.

Kuhusu hii riba, Gavana wa Benki Kuu anasema kuwa, baada ya tathmini wameona kuwa, kiwango kilichokuwepo cha asilimia 6 ya Riba ya Benki Kuu (CBR) kilikuwa bado kipo vizuri.

“Lakini, baada ya kufanya tathmini, tumeona tunaenda sasa kwenye msimu wa mavuno ambapo watu watahitaji kupata fedha zaidi kwa ajili ya ununuzi wa mazao na kuendelea na shughuli zao zingine.Kwa hiyo, ni kipindi ambacho kina uhitaji mkubwa wa fedha.”

Gavana Tutuba anasema kuwa, wanapopunguza kiwango cha CBR wanawezesha benki. “Kwa sababu kuna soko la fedha kati ya Benki Kuu na benki nyingine, japokuwa pia, kuna soko la fedha kati ya benki na benki,zinakopeshana."

Gavana Tutuba anafafanua kuwa, benki ili ipate fedha mara nyingi huwa inatumia utaratibu wa kukusanya dhamana kutoka kwa wananchi au ikatafuta fedha kutoka benki nyingine au kwenda Benki Kuu.

“Ndiyo chanzo cha fedha hizo, kwa hiyo maana yake ni kwamba sasa, benki zitapata fedha nyingi, zitaongeza sasa akiba ili kuendana na mahitaji ya soko, ndiyo maana tukafanya tathimini tukaona tunaenda kwenye msimu wa mavuno ambapo wananchi watahitaji namna ya kununuliwa mazao yao zaidi.

"Sasa, ni kuziwezesha benki zipate fedha nyingi zaidi, kusudi ziende zikasaidie wananchi wengi zaidi na zitoe mikopo mingi zaidi."

Gavana Tutuba anasema, hatua hii inawezesha benki kupata fedha nyingi ambazo zitasaidia kutoa mikopo kwa wananchi kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za maendeleo nchini.

Anasema kuwa, fedha hizo kutoka benki zitawafikia wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji katika uchumi baada ya kuomba mikopo benki au kuandika maandiko ya miradi.

Pia, Gavana Tutuba amefafanua kuwa, tathimini ambayo huwa inafanywa na kamati kabla ya kutoa maamuzi huwa inaangazia mwenendo wa uchumi wa dunia,mwenendo wa uchumi katika nchi za kanda zinazoijumuisha Tanzania na mwenendo wa uchumi hapa nchini.

Amesema,uamuzi huo wa kushusha riba hiyo unaakisi imani ya kamati katika mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5.

Gavana Tutuba amesema, hali hiyo inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuanza kwa msimu wa mavuno, pamoja na utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania.

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.

Wakati huo huo, amesema kuwa,uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika ukichochewa na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news