Waziri Mkuu wetu,hongera zifike kwako

NA LWAGA MWAMBANDE

JULAI 2,2025 Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametangaza rasmi kutokugombea tena ubunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, baada ya kulitumikia jimbo hilo kwa miaka 15.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao amekuwa mbunge wa jimbo hilo.
"Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili Kauli mbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana iweze kusonga mbele zaidi."

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,licha ya upendo wa Watanzania kwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amempongeza kwa uamuzi wa hekima na busara ambao ameuchukua huku akisisitiza kuwa,ataendelea kukumbukwa kwa kuwa kiongozi mahiri.Endelea;

¹Waziri mkuu wetu, hongera zifike kwako,
Mekuwa kinara kwetu, ukifanya kazi zako,
Sasa kwenye Bunge letu, wamaliza muda wako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

²Alishasema zamani, hata kumbukumbu ziko,
Ukiwa madarakani, unafanya ya mashiko,
Iingie akilini, kutambua muda wako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

³Miaka kumi na tano, mbunge Ruangwa huko,
Na tano ongeza tano, kwa nafasi uliyoko,
Muda unatosha mno, hayo maamuzi yako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

⁴Umefanya kazi zako, kwa huo uwezo wako,
Kwa zote nafasi zako, ulifanya ya mashiko,
Kweli kumbukumbu zako, zitazidia kuweko,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

⁵Kama Waziri Mkuu, takumbuka mambo yako,
Jinsi umekuwa juu, kwa usimamizi wako,
Wazembe wakuukuu, walionja joto lako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

⁶Ruangwa hawajachoka, ungelitaka kuweko,
Lakini unaondoka, na watu machozi yako,
Ni jema limetendeka, huo uamuzi wako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

⁷Msimamizi mahiri, ni moja ya sifa zako,
Kila jambo wahariri, ushahidi ukiweko,
Mefanya mengi mazuri, kapate mapumziko,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

⁸Nani asiyekumbuka, ufwatiliaji wako,
Jinsi walivyoumbuka, walioleta vituko,
Kula pesa kutibuka, sheria kuwa kiboko,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

⁹Sana tutakukumbuka, huo uongozi wako,
Na kila ukisikika, hayo matamko yako,
Vema umewajibika, acha pensheni iweko,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

¹⁰Ni mwanamichezo nguli, hiyo pia sifa yako,
Na tena kocha kamili, soka ni mapenzi yako,
Ona uwanja kamili, Ruangwa chagizo yako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

¹¹Darasa unalitoa, wanasiasa wenzako,
Muda wanaoutoa, wakitumikia huko,
Ya kwamba kujiondoa, ndio ukomavu wako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

¹²Ruangwa ajaye Bunge, mwanzo mwema takuwako,
Kwa Majaliwa atinge, na ushauri uweko,
Akienda akalonge, mazuri yenye mashiko,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

¹³Heri tunakutakia, kwenye ustaafu wako,
Uzidi kufurahia, pamoja na nyumba yako,
Huku ukitupatia, hiyo hekima ya kwako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

¹⁴Nawe ni historia, ukuu miaka yako,
Wawili mmetimia, na Sumaye kaka yako,
Kumi kututumikia, hongera kwake na kwako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

¹⁵Mungu alokuwezesha, kufanya mamuzi yako,
Azidi kupa maisha, furahia jasho lako,
Afya kikuneemesha, kwa miaka mingi yako,
Kung’atuka unapendwa, hilo jambo la maana.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news