DODOMA-Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa maeneo ambayo yamepata fedha nyingi kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) ambapo umepokea zaidi ya shilingi bilioni 36.596.
Fedha hizo ambazo zimetolewa na serikali zimetumika kujenga shule mpya 41 za sekondari ambazo miongoni mwake ni pamoja na shule moja ya wasichana, shule moja ya kanda ya wavulana, shule za kata 36, shule moja ya amali ya mkoa na shule mbili za amali za kata.
Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma,Mwalimu Vicent Kayombo amesema kuwa, fedha hizo pia zimetumika kujenga Madarasa 77, Matundu ya Vyoo 119, Maabara 19, Mabweni 22, na Nyumba za Walimu 22.
Mwalimu Kayombo amesema kuwa, Mkoa wa Dodoma umejenga shule mpya ya wasichana Manchali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.450 sambamba na ujenzi wa shule mpya ya Amali ya mkoa iliyojengwa katika kijiji cha Manchali wilayani Chamwino kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.6.
Mwalimu Kayombo ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika mkoa wa Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ambazo zitapunguza umbali wa wanafunzi kwenda shuleni ikiwa ni pamoja na kuondokana na vishawishi njiani, na kuongeza muda wa wanafunzi kujisomea.



