Tanzania yaikaribisha Korea Kusini kushiriki miradi mikubwa ya miundombinu

DAR-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuonesha dhamira ya dhati kuvutia uwekezaji wa kimataifa kupitia semina ya kimkakati iliyowakutanisha viongozi wakuu wa serikali na wawekezaji kutoka Korea Kusini.
Semina hiyo maalum ilifanyika Julai 24, 2025 katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, ikiandaliwa na Taasisi ya Fedha ya Korea kwa ajili ya Ujenzi (K-Finco) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewashawishi wawekezaji wa Korea kushiriki kwa dhati katika miradi ya kimkakati ya maendeleo ya ardhi, nyumba na miundombinu nchini Tanzania.
“Tunajenga taifa kwa msingi wa haki katika umiliki wa ardhi, usawa wa kijamii na ukuaji wa miji yenye mpangilio. Tunahitaji ushirikiano wenu ili kufanikisha haya,” alisema Mhe. Ndejembi. Alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi salama na wazi kwa uwekezaji, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia sera thabiti, mifumo ya kidijitali na utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa uwazi na tija.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Togolani Mavura, aliwahimiza wawekezaji kuangazia fursa lukuki zilizopo nchini Tanzania katika sekta za reli, bandari, barabara, viwanja vya ndege na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Awali, Balozi wa Korea nchini Tanzania alifungua rasmi semina hiyo kwa kusisitiza kuwa Korea iko tayari kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania, hasa katika sekta ya ujenzi na miundombinu.
Aliahidi kuwa Serikali ya Korea itaendelea kuhamasisha kampuni zake kuwekeza nchini Tanzania kwa nia ya kushirikiana katika kuharakisha maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news