Tanzania yaipongeza Canada kwa kuchangia miradi ya maendeleo ya elimu

DODOMA-Serikali ya Tanzania imeipongeza Serikali ya Canada kwa jitihada zake za kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo miradi ya elimu na maendeleo ya rasilimali watu.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo yake na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Mhe. Sandeep Sarai ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma Julai 21, 2025, Mhe. Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali ya Canada imeendelea kushirikiana na Tanzania katika kuchangia miradi mbalimbali ya elimu ikiwemo Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) ambapo Canada imetoa Shilingi Bilioni 92 kwa Tanzania kwa ajili ya kuendeleza vyuo mbalimbali.
Aidha, amesema Canada imeendelea kusaidia elimu ya ufundi nchini ambapo nchi hiyo kupitia mradi wa uwezeshaji wa ujuzi (ESP) wenye thamani ya dola za Canada milioni 25 sawa na Shilingi Bilioni 47 ambapo mradi huu umejikita katika kuboresha vyuo 12 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) vya hapa nchini.

Kadhalika ameongeza kusema kuwa amefurahishwa na kuanzishwa kwa mradi mpya unaolenga kuleta maendeleo endelevu katika elimu ya ualimu (TESDP) kwa kuhusisha vyuo vya ualimu vya Serikali pamoja na Vyuo vya Elimu ya Ufundi na mafunzo ya ufundi Stadi yaani TVET kupitia VETA wenye thamani ya Dola za Canada milioni 19.5 sawa na Shilingi Bilioni 37.

Pia ameishukuru Serikali ya Canada kwa uwekezaji mkubwa wa Dola za Kimarekani Milioni 12 katika Mpango wa Lishe katika Shule za hapa nchini unaoratibiwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambao unalenga kuboresha mahudhirio na afya za wanafunzi ambao utatekelezwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
“Ni matarajio yetu kuwa mradi huu utaendelezwa hata katika mikoa mingine,” alisema Prof. Mkenda.

Mhe. Prof. Mkenda pia ameipongeza Serikali ya Canada kwa kuwekeza Dola za Kimarekani Bilioni 20 katika Mradi wa BLOOM Afrika unaotekelezwa na Shirika lisilo la kIserikali la World Vision kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na wasichana waliopo pembezoni kupitia mafunzo ya ujuzi chini ya Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi (VETA)

“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na Canada inayoenda zaidi ya Sekta ya Elimu kwani yapo maeneo mengi tunayoshirikiana na Canada. Tunafurahi sana mgeni wetu kututembelea na tunamkaribisha Tanzania,” alisisitiza Prof. Mkenda.
Kwa upande wake, Mhe. Sarai amesema kuwa, Tanzania na Canada zimeendelea kushirikiana kwa zaidi ya miongo sita katika sekta mbalimbali za Elimu, Afya, utunzaji mazingira na nyinginezo na kwamba ziara yake inalenga katika kuimarisha ushirikiano huo wa kihistoria.

Ameongeza kuwa, Serikali yake, itaendelea kuchangia sekta zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja ikiwemo elimu ambapo pia alitumia fursa hiyo kutangaza ufadhili kwa miradi mipya itakayojikita katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Miradi hiyo ni pamoja na Mpango wa Lishe kwa mikoa ya Lindi na Mtwara wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 12, Mradi wa BLOOM kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na wasichana waliopo pembezoni wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 20.
Wakati huohuo, Mhe. Sarai katika ziara yake jijini Dodoma alikitembelea Kituo cha Afya cha Makole, Kiwanda cha Asali cha Central Park Bees, Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Kampuni ya Kusindika Unga wa Sembe ya Chamwino.

Mhe. Sarai yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 20 hadi 23 Julai, 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news