TEA kupitia Mfuko wa SDF ilivyomuongezea mwendo wa mafanikio mjasiriamali wa viungo vya chakula

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) umeendelea kuacha alama kwa wanufaika waliopata mafunzo ya ujuzi katika sekta mbalimbali.

Wakati wa utekelezaji wa mafunzo ya kuendeleza ujuzi, Mfuko wa SDF ulifadhili mafunzo kwenye sekta sita za kipaumbele ambazo ni TEHAMA, Uchukuzi, Utalii na Huduma za Ukarimu, Ujenzi, Nishati na Kilimo Uchumi.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi, lengo likiwa ni kuwafikia watanzania wengi zaidi kwenye maeneo yao.

Miongoni mwa wanufaika hao kupitia mafunzo yaliyotolewa na SIDO mkoani Iringa kwa ufadhili wa SDF ni Geshom Juma Munyi kutoka mkoani Iringa ambaye ni mjasiriamali anayejihusisha na usindikaji wa viungo vya chakula.
Katika mazungumzo na DIRAMAKINI ndani ya banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) lililopo katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam leo Julai 2,2025, Munyi amekiri kuwa, TEA imemuongezea mwendo wa mafanikio.

Viungo ambavyo anasindika ni pamoja na mdalasini, iliki, karafuu, pilipili manga, chai tiba na mchanganyiko mbalimbali wa viungo (tangawizi mix) ambayo imechanganyika na tangawizi, asali, vitunguu swaumu.

“Ujuzi huu wa usindikaji nimejifunza nikiwa pale Iringa Mjini kupitia wadau wanaoitwa SIDO, na nipo kwenye banda la TEA kwa sababu mafunzo niliyopata Iringa Mjini kupitia SIDO yaliwezeshwa na TEA kupitia Mfuko wa SDF (Skills Development Fund).

"Kupitia TEA, walifadhili mafunzo hayo kwa kutupatia walimu kwa ajili ya kutufundisha, pale pale SIDO na waliwezesha mazingira kwa maana kwamba majengo, mashine na kila kitu ambacho kinahusiana na mafunzo.

"Kwa hiyo, mimi kwa upande wangu nilifanikiwa kujifunza mambo ya usindikaji wa viungo, kwa hiyo licha ya kusindika viungo, lakini huwa pia ninauza malighafi kama tangawizi kutoka shambani moja kwa moja, tangawizi iliyokaushwa na tangawizi ya unga."
Amesema, ujuzi huo aliupata kutoka SIDO kupitia Mradi wa SDF chini ya TEA. Munyi anakiri kuwa, ujuzi huo licha ya kumpa uwanda mpana wa kusindika viungo mbalimbali kwa ajili ya chakula, pia umemuwezesha kupata soko kubwa ndani na nje ya nchi.

“Kwa hiyo, huwa ninauza kwa wingi hata ikifika tani moja ninauza, nilishabahatika pia kuuza nchini Afrika Kusini na Zambia hadi tani 20.Kwa hiyo, mimi nimeamua kujikita kwa upande huo, kwa ukubwa huo ili niweze kuendesha maisha yangu.”

Vilevile, mjasiriamali na msindikaji huyo anathibitisha kuwa, moyo wa upendo na hamasa kutoka kwa watumishi wa TEA umeendelea kumuongezea hatua ya mafanikio yake katika kuyaendea malengo makubwa zaidi.

“Kwanza wafanyakazi wenyewe ambao wanauendesha mfuko, wamekuwa watu ambao wananitia moyo sana na kila siku huwa wanatamani kujua hatua zangu,lengo likiwa ni kuona ninafanya vizuri zaidi, hao ni watumishi wa TEA.”

Aidha, amesema kuwa, Mfuko wa SDF licha ya kufanikisha yeye kupata ujuzi umemuwezesha kukutana na wadau mbalimbali ambao wanahusika na biashara yake hiyo.

Miongoni mwa wadau hao, Munyi amewataja kuwa, ni wakulima wakubwa, wanunuzi wakubwa ambao pia wanatoka katika taasisi na mashirika makubwa ya Serikali.

“Kwa hiyo, TEA wana jitihada kubwa sana za kuhakikisha mnufaika wao anasonga mbele, hawapendi kuona unakosa kitu.

“Kwa mfano hata hapa katika haya maonesho ya Sabasaba wanaweza kutoka kwenye banda wakaenda kunitafutia wateja,wakaniletea, wakanitambulisha, nikaongea na wateja na kuwahudumia.”

Jambo lingine ambalo Munyi analisisitiza zaidi ni kwamba, Mfuko wa SDF umemuwezesha kupata elimu ambayo ni uwekezaji tosha katika maisha yake.

Amefafanua kuwa, elimu hiyo imempa mwanga wa kutosha kuhusu namna ya kuboresha, na kusindika viungo mbalimbali vya chakula.

Jambo kubwa zaidi, anasema, TEA imekuwa dira kwake, kwani pia imekuwa ikimsaidia kushiriki maonesho mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.

Kutokana na mchango mkubwa wa mfuko huo katika miradi inayostawisha jamii na kuboresha hali zao za kiuchumi, Munyi ametumia nafasi hiyo kuwashirikisha wadau na Serikali jambo.

“Wito wangu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa maendeleo, ninawaomba waendelee kuuwezesha huu mfuko wa SDF ili uendelee kufadhili miradi ambayo inaacha alama chanya kwa maisha ya wananchi wengi kama ulivyofanya kwangu.
Amesema, mafanikio ya kutekeleza miradi ambayo inaibua vipaji vya vijana kama yeye si tu kwamba inasaidia kuboresha uchumi wake, bali pia ni fursa mpya ya ajira kwa vijana na wategemezi wao.

“Kwa hiyo, huu mfuko ilibidi uwe endelevu kwa sababu vijana wanaotoka chuoni ni wengi sana, kuna diploma, kuna cheti, kuna degree yaani ni wengi, kwa hiyo ni vema mfuko ukawa endelevu na siyo kama mradi ambao unaweza ukaisha miaka miwili, vipi kuhusu wale waliopo nyuma.”

Anasema, kufanikiwa kwake, kila mmoja anatamani kupata ujuzi wa namna hiyo, ingawa anasaidia kwa sehemu yake, lakini si kwa matokeo bora kama TEA walivyofanya kwao.
"Kwa kweli, TEA waendelee kutuunga mkono kwa sababu mimi ninazalisha hizi bidhaa, lakini nikikuwa kwa ukubwa ule ambao mimi ninautaka miaka kadhaa ijayo nitakuwa mzalishaji mkubwa zaidi nchini.”

Amesema, ndoto zake ni kurudisha shukrani kwa TEA na Serikali katika kuendesha uzalishaji ambao utaajiri Watanzania wengi na kuchangia pato la jamii na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news