Waguswa na mchango wa TEA katika kusaidia Serikali kuendeleza elimu nchini

NA GODFREY NNKO

WANANCHI mbalimbali wameendelea kuipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kutokana na mchango wake muhimu unaosaidia kutatua changamoto za elimu nchini.
Pongezi hizo wamezitoa kwa nyakati tofauti Julai 2,2025 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.

"Kwa ujumla TEA ni taasisi muhimu sana katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuinua ubora na kuongeza upatikanaji wa elimu kwa usawa nchini,hivyo niwapongeze kwa kazi yao kubwa, kikubwa tuendelee kuwashika mkono ili waweze kuyafikia maeneo mengi zaidi,"amesema mkazi wa Dar es Salaam na mdau wa elimu nchini ambaye ameshiriki katika maonesho hayo.
Mdau huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe anasema kuwa,michango ya hiyari kutoka kwa wananchi na wadau wa maendeleo itawezesha TEA kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali ya elimu nchini.

Naye Salha Said mkazi wa Mabibo amesema kuwa,kazi kubwa inayofanywa na TEA katika kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa inapaswa kuungwa mkono ili iwe na rasilimali fedha za kutosha.

"Kila mradi unahitaji fedha, hivyo ili TEA iweze kutimiza malengo ya kuzifikia shule nyingi zaidi, sisi Watanzania na wadau wa elimu tuna wajibu wa kutunisha Mfuko wa Elimu wa Taifa ili uwe na rasilimali fedha za kutosha na endelevu."
Afisa Uhusiano na Mahusiano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),Eliafile Solla amesema kuwa,TEA ni miongoni mwa taasisi za umma ambazo zimeshiriki maonesho hayo ambayo yanaongozwa na kauli mbiu ya Fahari kwa Tanzania.

"Maonesho haya ni muhimu sana kwa TEA kwa sababu ni jukwaa ambalo linaikutanisha TEA na wadau wa aina mbalimbali."

Bi.Solla anafafanua kuwa,TEA ina jukumu kubwa la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao una majukumu makuu mawili.
Ameyataja majukumu hayo kuwa ni kutafuta rasilimali fedha na vifaa kutoka kwa wadau mbalimbali ambao wamewafuata Maonesho ya Sabasaba.

"Kwa hiyo,tumeamua kutoka sasa kwenda kuwatafuta wadau,pili tuweze kujitangaza na kutangaza mafanikio yetu ambayo tumeyapata ndani ya kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita."

Ameendelea kufafanua kuwa,TEA kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa umetekeleza mambo mengi nchini ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya elimu.
Vilevile, TEA kupitia mfuko huo imejenga maabara za sayansi, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, mabweni na matundu ya vyoo.

Pia, imeshiriki kuboresha mazingira mengine ambayo yanamuwezesha mwalimu na mwanafunzi kufikia malengo yake katika hali ya ujifunzaji na ufundishaji.
"Kwa hiyo, TEA tumeamua sasa kutoka ofisini kuja Sabasaba lengo likiwa ni kuwafuata wananchi huku waliko."

Amesema, kupitia maonesho hayo kuna wadau wengi kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo uwepo wao unawapa fursa ya kukutana na wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
"Lakini,pia tunakutana na wadau wengi sana ambao wanatamani kujua Serikali imefanya nini katika maendeleo au mazingira ya elimu kwa maana ya ujifunzaji na ufundishaji."

Bi.Solla anasema, uwepo wa TEA viwanja vya Sabasaba kumewapa fursa ya kuwashirikisha wadau umuhimu wa kuchangia Mfuko wa Taifa wa Elimu.
Miongoni mwa faida za wachangiaji wa mfuko huo ni pamoja na kupata nafuu ya kodi katika kodi ya mapato kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Aidha,mchangiaji wa mfuko huo kupitia TEA anapata nafasi ya kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, kwani huandikwa katika rejista ya kudumu ya wachangiaji.
Mchangiaji pia, huwa anapatiwa hati au barua ya utambuzi wa uchangiaji wa elimu nchini.

TEA ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya mwaka 2001 chini ya kifungu cha 5 (1) ili kuratibu na kusimamia Mfuko wa Taifa wa Elimu.
Mfuko huo ulianzishwa kwa sheria hiyo hiyo, kwa lengo la kusaidia harakati za Serikali katika kuendeleza elimu nchini.Mamlaka hii, pia ipo chini ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news