DAR-Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam wametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.
Shule zilizoshiriki katika ziara hiyo ni Shule ya Sekondari Wailes, Shule ya Sekondari Mwinyi, Shule ya Msingi Upendo, na Shule ya Msingi Kibamba ‘B’.
Kupitia ziara hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kuhusu majukumu mbalimbali ya Benki Kuu ya Tanzania, yakiwemo utekelezaji wa sera ya fedha, usimamizi wa sekta ya fedha, pamoja na usimamizi wa mifumo ya malipo ya Taifa.
Aidha, walielimishwa juu ya utambuzi wa alama za usalama katika noti halali, matumizi sahihi ya huduma za kifedha, na umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa kujiwekea akiba.
Vilevile, walifahamishwa kuhusu kazi zinazofanywa na Kitengo cha Mapambano dhidi ya Utakasishaji Fedha Haramu, taratibu za ajira ndani ya Benki Kuu, pamoja na mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu cha Tanzania.
Benki Kuu inatumia maonesho haya kama jukwaa la kuelimisha umma, hususan wanafunzi, kuhusu masuala ya fedha kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha katika maisha yao ya sasa na baadaye.







